Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa klabu ya PSG ya Ufaransa, Neymar (pichani) yuko mbioni kwenda Saudi Arabia kujiunga na klabu ya Al Hilal ambayo hivi karibuni ilikwama kumsajili Lionel Messi.
Iwapo mpango huo utafanikiwa, Neymar ataungana na mastaa wengine waliowahi kutamba Ulaya kabla ya kutimkia Saudi Arabia akiwamo Cristiano Ronaldo ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Al Nassr.
Wawakilishi wa Al Hilal tayari wametua katika jiji la Paris nchini Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo ya kumshawishi mchezaji huyo aachane na PSG na kwenda kucheza soka Saudi Arabia.
Ronaldo hivi karibuni alisema anaamini wachezaji wengi mastaa wa Ulaya watakwenda kucheza soka Saudi Arabia baada ya yeye kufanya hivyo akisisitiza kwamba ligi ya nchi hiyo itakuwa bora na maarufu duniani.
Mpango wa Messi kwenda Saudi Arabia ulikwama hivi karibuni baada ya mchezaji huyo kuamua kujiunga na Inter Miami ya Marekani licha ya imani iliyokuwapo kwamba angejiunga na klabu yake ya zamani ya Barcelona au angekwenda kujiunga na Al Hilal.
Inaonekana baada ya kumkosa Messi, Al Hilal sasa imeamua kumgeukia Neymar ambaye kabla ya kuanza msimu wa 2022-23, alinukuliwa akidai kwamba haijui hatma yake PSG lakini baada ya msimu kuanza akapata mafanikio kabla ya kuumia na sasa hadithi ya kutaka kuhama ikaanza kuibuka upya.
Klabu nyingine ambazo zimewahi kudaiwa kumtaka Neymar ni Newcastle na Chelsea, awali Barcelona nayo ilitajwa kabla ya kocha wa timu hiyo Xavi kukanusha jambo hilo.
Kimataifa Neymar kumfuata Ronaldo Saudi Arabia
Neymar kumfuata Ronaldo Saudi Arabia
Read also
