Na mwandishi wetu
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeweka wazi kuwachukulia hatua wote ambao hawatahudhuria hafla ya utolewaji wa tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa mwaka huu.
Hafla hiyo inatarajia kufanyika Jumatatu hii jijini Tanga, siku ambayo mchezo wa fainali wa Kombe la FA kati ya Azam na Yanga utachezwa pia kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Kupitia taarifa yake maalum, bodi hiyo imekumbusha kuwa mteule yeyote wa kipengele cha kwenye tuzo hizo atakayeshindwa kuhudhuria bila ridhaa ya TFF au TPLB atachukuliwa hatua za kinidhamu kama kutozwa faini, kufungiwa mechi na kupoteza nafasi ya ushindi pia.
Imeelezwa kuwa hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 11:9 kama inavyofafanua: “Mhusika yeyote aliyeteuliwa katika orodha ya wanaowania Tuzo za Ligi Kuu anawajibika kufuata maelekezo ya TFF kwa ajili ya Tuzo za Ligi Kuu ikiwemo ulazima wa kuhudhuria sherehe za tuzo.
“Mteule yeyote anayewania Tuzo za Ligi Kuu atakayeshindwa kufuata utaratibu, maelekezo na kuhudhuria sherehe za tuzo bila ridhaa ya TFF/TPLB atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo faini, kufungiwa michezo au kipindi fulani pamoja na kupoteza nafasi ya kuwa mshindi na nafasi yake kuchukuliwa na mshindani anayemfuatia kutokana na vigezo.”
Tuzo hizo zinazosubiriwa kwa hamu zitahusisha makundi matano ambayo ni Tuzo za Kombe la FA (ASFC), Tuzo za Ligi Kuu Bara, Tuzo za Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL), Tuzo za Utawala na Tuzo za ligi nyingine kama Championship, First League na ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
Soka Asiyehudhuria tuzo za TFF kuadhibiwa
Asiyehudhuria tuzo za TFF kuadhibiwa
Read also
