Na Hassan Kingu
Huo ndio ukweli, mechi za mwisho za Ligi Kuu NBC zinanogeshwa na vita ya Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza kwenye tuzo ya mfungaji bora, ukiacha vita kali ya kujinasua na janga la kushuka daraja.
Mechi hizo zinapigwa leo Ijumaa saa tisa na nusu alasiri, tuzo ya kuwania kiatu cha mfungaji bora ghafla imegeuka kuwa mpambano wa Mayele na Ntibazonkiza.
Ntibazonkiza amebadili upepo ghafla kwa mabao yake matano aliyofunga katika mechi dhidi ya Polisi Tanzania na hivyo kufikisha mabao 15 akizidiwa bao moja na Mayele.
Na ingawa Ntibazonkiza amenukuliwa na GreenSports akisema hashindani na Mayele lakini si kweli kwamba haitaki tuzo ya mfungaji bora, atapambana kuhakikisha anafunga ili kuibuka mfungaji bora na hiyo maana yake ni kwamba yupo vitani.
Katika hali ya kawaida wachezaji wenzake wa Simba pia watapenda kuona anaibuka mfungaji bora, penalti, mipira ya adhabu na mazingira yote ya kupata bao watampa yeye ili aibuke mfungaji bora na kumbwaga Mayele ambaye kila mtu aliamini msimu huu tuzo hiyo ni mali yake.
Leo Yanga inakamilisha mechi yake ya mwisho ya ligi dhidi ya Prisons wakati Simba itaivaa Coastal Union, kama tutazichukulia mechi hizi kwa kuangalia yaliyopita, mashabiki wa Simba wana kila sababu ya kujipa matumaini kwamba mchezaji wao Ntibazonkiza ataibuka mfungaji bora na wale wa Yanga wataingiwa na huzuni na wasiwasi kwamba Mayele ataikosa tuzo hiyo kwa mara ya pili.
Prisons wamekuwa wagumu kwa Yanga wakati Coastal wanajulikana ni vibonde wa Simba, haitokuwa ajabu Simba kuifunga Coastal hata mabao matano na Yanga haitokuwa ajabu kutoka sare na Prisons.
Mazingira hayo hata hivyo hayana jibu la moja kwa moja kwamba nani ataibuka kinara wa mabao msimu huu, lolote linaweza kutokea katika mechi hizo za kufunga msimu.

Msimu uliopita wa 2021-22 Mayele alipoteza tuzo hiyo katika hatua za mwisho mbele ya George Mpole na msimu huu anatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwa hali hiyo kwani kwa hatua iliyofikia anaweza akashangazwa tena msimu huu wa 2022-23.
Matarajio yote makubwa ya awali yakafutika na badala yake akaishia nafasi ya pili kama ilivyokuwa msimu uliopita, chanzo cha yote ni huyu mtu anayeitwa Ntibazonkiza ambaye alikuwa naye Yanga kabla ya kutimuliwa na sasa anaelekea kuzima ‘mitetemo’ ya Mayele katika hatua za mwisho.
Ntibazonkiza ambaye alijiunga na Simba akitokea Geita Gold katika dirisha dogo, mabao yake mengine aliyafunga akiwa na timu hiyo, ametokea kuwa moto tangu atue Simba, si kwa kufunga mabao tu bali pia amekuwa mpishi muhimu wa mabao ya timu hiyo.
Ukiachana na Mayele na Ntibazonkiza janga la kujinasua na hatari ya kushuka daraja nalo lina vita yake inayohusisha timu za Mbeya City, iliyo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 31, KMC ya 14 pointi 29, na Polisi Tanzania ya 15 pointi 25 na Ruvu Shooting ya 16 pointi 20.
Matokeo ya mechi za leo pia ndiyo yatakayoamua timu ipi itacheza play-off, zilizo katika hatari hiyo ni KMC, Coastal Union, Mbeya City na Mtibwa Sugar.
Mechi za leo Ijumaa za Ligi Kuu NBC ni kama ifuatavyo…
Prisons v Yanga
Simba v Coastal
Azam v Polisi Tanzania
Namungo v Singida Big
Ihefu v Kagera
Mbeya City v KMC
Mtibwa Sugar v Geita Gold
Ruvu Shooting v Dodoma Jiji
