Barcelona, Hispania
Hatimaye, Lionel Messi ametangaza rasmi kwamba anaelekea nchini Marekani kujiunga na klabu ya Inter Miami FC na hivyo kumaliza mjadala juu ya hatma yake baada ya kuihama PSG ya Ufaransa.
Messi katika siku za karibuni amekuwa katika mjadala kuhusu hatma yake baada ya kuihama PSG huku akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia pamoja na kurudi klabu yake ya zamani ya Barcelona.
Baba mzazi wa Messi, Jorge Messi ambaye pia anafanya kazi ya uwakala wa mchezaji huyo aliwahi kunukuliwa akisema kwamba mtoto wake anapenda na yuko tayari kurudi Barca.
Messi aliihama Barca Agosti 2021 akiwa mchezaji huru na kujiunga na PSG kwa sababu Barca haikuruhusiwa kumpa mkataba mchezaji huyo kwa mujibu wa kanuni za fedha za La Liga.
Barca ilikuwa tayari kumsajili Messi msimu huu na tayari kocha wa timu hiyo, Xavi alisema kwamba walikuwa tayari kwa jambo hilo lakini sasa ni wazi mpango huo umekwama sababu inatajwa kuwa ni ile ile ya kanuni ya matumizi ya fedha.
“Nilipenda sana kurudi Barca, lakini sitaki kurudia hali ile ile niliyokutana nayo wakati naondoka,” alisema Messi mara baada ya kufikia makubaliano na klabu ya Inter Miami.
Messi alisema baada ya kusajiliwa PSG aliishi hotelini katika jiji la Paris, na watoto wake pia walikuwa wakienda shule wakitokea hotelini na kwamba hawakutaka kwenda Paris lakini mazingira yaliwalazimu kukubaliana na hilo.
Kimataifa Messi atangaza kuhamia Marekani
Messi atangaza kuhamia Marekani
Read also
