Na mwandishi wetu
Kiungo mpya wa Azam FC, Feisal Salum, ‘Fei Toto’ amemshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kulimaliza suala lake na kufanikiwa kujiunga na kikosi cha Azam.
Hayo ameyasema leo Alhamisi kwenye makao makuu ya klabu hiyo Mzizima, wakati akitambulishwa baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia timu hiyo ambayo amekuwa akihusishwa nayo kwa muda mrefu.
“Namshukuru sana Rais Samia kwa kuliingilia suala hili Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi katika majukumu yake, nafurahi kujiunga na Azam na nitahakikisha napiga kazi kuwapa furaha pia naishukuru Yanga, ingawa nimeondoka lakini bado naipenda,” alisema Fei Toto.
Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema usajili wa Fei Toto unakwenda kuimarisha kikosi chao ambacho msimu ujao wamedhamiria kufanya makubwa katika mashindano ya ndani na nje ya Tanzania.
Alisema wana imani kubwa na mchezaji huyo ambaye kwenye kikosi chao atarahisisha kufikia malengo ambayo wamekuwa nayo kwa misimu kadhaa nyuma kwa kushirikiana na wachezaji wengine wapya wanaotarajia kuwasajili kwenye dirisha kubwa na wale waliopo kwenye kikosi chao.
Azam imekamilisha dili hilo baada ya kuelezwa kukutana na Yanga tangu juzi ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia kupeleka ombi kwa Yanga akiwataka wamalize mgogoro wao na mchezaji huyo.
Fei Toto alishinikiza kuvunja mkataba wake na Yanga tangu Desemba, mwaka jana kabla ya Yanga kuamua kudai haki yake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaamuru mchezaji huyo arejee Yanga kabla ya kiungo huyo kupinga na kujipanga kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Kitendo cha Fei kutua Azam pia kimezima safari ya kwenda Cas ambako alichangisha kiasi cha pesa kwa Watanzania takriban Sh milioni 109 ambazo amesema atazipeleka nyumba za ibada na nyingine atazipeleka kwenye nyumba za kulea watoto yatima.
Fei ametambulishwa Azam na kukabidhiwa jezi namba sita ambayo ni jezi yake pendwa aliyokuwa akiitumia tangu alipokuwa Yanga na hata timu ya taifa, Taifa Stars.
Awali Yanga walitoa taarifa ya kuachana na mchezaji huyo baada ya wao kufikia makubaliano na klabu ya Azam ingawa hawakutaja kiasi cha fedha walicholipwa hadi kumuachia mchezaji huyo ambaye awali walionekana kutokuwa tayari kuvunja naye mkataba.