Madrid, Hispania
Mahakama ya Madrid imewapa adhabu za faini na marufuku ya kwenye viwanja vya soka watu saba kwa makosa ya kumfanyia dhihaka za ubaguzi wa rangi mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior.
Kati ya watu hao wanne wametozwa faini ya Dola 51,700 na kupigwa marufuku kwenye viwanja vya soka kwa miaka miwili kwa kosa la kuweka sanamu ya kuuzia nguo yenye mfanano wa Vinicius Jr nje ya uwanja wa mazoezi wa klabu ya Real Madrid.
Watu hao ambao walihukumiwa jana Jumatatu wanadaiwa kufanya kosa hilo Januari mwaka huu, walikamatwa siku 11 zilizopita kabla ya hukumu hiyo na kuachiwa kwa dhamana na mahakama hiyo.
Katika kundi hilo watu wengine watatu walitozwa faini ya Dola 4,300 na kupigwa marufuku kuingia kwenye viwanja vya soka kwa mwaka mmoja kwa kosa la kutoa kauli na ishara za ubaguzi wa rangi kwa Vinicius Jr wakati wa mechi kati ya Real Madrid na Valencia iliyochezwa Mei 21 mwaka huu.
Watu hao ambao umri wao ni kati ya miaka 18 na 21 walikamatwa na kuwekwa ndani siku mbili baada ya mechi hiyo.
Katika siku za hivi karibuni, Vinicius Jr amekuwa akikumbana na kadhia ya kufanyiwa dhihaka za ubaguzi wa rangi na aliwahi kuzilalamikia mamlaka Hispania kutochukua hatua kali dhidi ya wahusika na kuna wakati alinukuliwa akisema kwamba ligi ya Hispania ni mali ya wabaguzi wa rangi.
Matukio hayo yameigusa hadi Serikali ya Brazil nchi anayotokea Vinicius Jr ambayo imetaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wanaohusika na vitendo vya ubaguzi wa rangi kwenye soka.
Kimataifa Waliomdhihaki Vinicius Jr wahukumiwa
Waliomdhihaki Vinicius Jr wahukumiwa
Read also
