Madrid, Hispania
Straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane anaongoza orodha ya wachezaji wanaotakiwa Real Madrid ili kuziba pengo la Karim Benzema ambaye anatimkia Saudi Arabia na jana Jumapili aliagwa rasmi.
Kane (pichani) ameifungia Spurs mabao 280 katika mechi 435, ana mwaka mmoja katika mkataba na Spurs lakini kwa siku za karibuni amekuwa akitajwa kuwa na nia ya kutafuta changamoto mpya katika klabu nyingine.
Baadhi ya klabu ambazo amekuwa akihusishwa nazo Kane ukiacha Real Madrid ni Bayern Munich, PSG na Man United lakini tangu kuibuka habari za kuondoka kwa Benzema, Real Madrid inadaiwa kuongeza nguvu katika mbio za kumtaka mchezaji huyo.
Kane mwenye umri wa miaka 29 bado hajasema lolote kuhusu klabu anayotaka kujiunga nayo lakini kilicho wazi ni kwamba azma ya kuihama Spurs amekuwa nayo kwa muda mrefu na hapana shaka atapenda kuhamia Real Madrid.
Ukiacha Kane wachezaji wengine ambao Real Madrid inawawinda ni Victor Osimhen wa Napoli, Kai Havertz wa Chelsea, Dusan Vlahovic wa Juventus na Lautaro Martinez wa Inter Milan.
Kati ya wachezaji wote hao jina la Kane ndilo linaloongoza orodha hiyo na matumaini yaliyopo ni kwamba kuondoka kwa baadhi ya mastaa katika klabu hiyo kutasaidia kurahisisha usajili wa Kane ambaye pia ni nahodha na mshambuliaji tegemeo wa timu ya Taifa ya England.
Ukiacha Benzema, wachezaji wengine wanaoondoka Real Madrid ni pamoja na Marion Diaz, Eden Hazard na Marco Asensio.
Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy anapenda kumbakisha Kane katika klabu hiyo ya utotoni ingawa inaeleweka kwamba atapenda kufanya biashara na kutaka Pauni 100 milioni ambazo hapana shaka Real Madrid watajenga hoja ili wapunguziwe.
Wakati nguvu ikiwekwa katika usajili wa Kane, Real Madrid pia ipo katika mazungumzo yanayodaiwa kwenda vizuri ya kumsajili kiungo wa England na klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, Jude Bellingham.
Kimataifa Kane kumrithi Benzema Real Madrid
Kane kumrithi Benzema Real Madrid
Read also
