Milan, Italia
Hatimaye mshambuliaji mkongwe wa AC Milan na timu ya Taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 41, jana Jumapili alitangaza rasmi kustaafu soka.
Mkataba wa Ibrahimovic na AC Milan unafikia ukomo mwisho wa mwezi huu hivyo hatoongeza tena mkataba huku sababu ikitajwa kuwa ni janga la kuwa majeruhi mara kwa mara na ndilo lililomfanya aamue kustaafu.
Akiwa katika mkutano na waandishi wa habari jana, Ibrahimovic alisema hakuna mtu yeyote aliyekuwa akifahamu mpango wake wa kutangaza uamuzi huo mkubwa wa kuachana na soka la ushindani.
“Hata familia yangu haikuwa ikijua jambo hilo, nilitaka wakati natangaza kila mtu asikie hapo hapo na wakati huo huo,” alisema mshambuliaji huyo aliyewahi kucheza soka katika klabu mbalimbali za Ulaya.
Katika maisha yake na AC Milan, Ibrahimovic ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 93 katika mechi 163 na ameichezea vipindi viwili tofauti akirudi mara ya mwisho Januari 2020 na kuiwezesha kubeba taji la Serie A mwaka jana likiwa ni taji lake la pili na timu hiyo.
Ibrahimovic (pichani juu) alionekana akilengwa na machozi hasa alipoliona bango la mashabiki lililoandikwa ‘Kwaheri’ huku wakiimba jina lake na kumshangilia, aliwapungia mkono huku machozi yakimlenga.
Akiwaaga mashabiki wa Milan Ibrahimovic alisema, “Nina kumbukumbu nyingi na matukio ya kufurahisha katika uwanja huu, mara ya kwanza nilipokuja hapa mlinipa furaha na safari hii mmenipa upendo.”
Ibrahimovic alianza kutamba na klabu ya Malmo FF ya Sweden mwaka 1999 na kutua Ajax ya Uholanzi mwaka 2001 na baada ya hapo akatamba na klabu za AC Milan, Inter Milan, Barcelona, PSG pamoja na Manchester United.
Kwa upande wa timu ya Taifa ya Sweden, ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa na mabao 62 na ameichezea mechi 121, alistaafu timu hiyo mwaka 2016 kabla ya kurudi mwaka 2021 akipania kusaidia kufuzu Kombe la Dunia 2022 lakini alikwama.
