Algers, Algeria
Yanga imeshindwa kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kubeba Kombe la Shirikisho Afrika licha ya kuilaza USM Algers bao 1-0 katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Vinara hao wa Ligi Kuu NBC wakiwa ugenini Algeria Jumamosi hii walipambana kishujaa na kupata bao hilo pekee la mkwaju wa penalti lililofungwa na Djuma Shaban katika dakika ya saba baada ya Kennedy Musonda kuchezewa rafu.
Wenyeji USMA walineemeka na bao la ugenini baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na hivyo matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Katika mechi hiyo kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alianza kwa mfumo wa 3-4-3, ambao ulionekana kuwa na faida kwa timu yake hadi kupata bao hilo pekee.
Yanga pia iliweza kufanya mashambulizi ya maana kwenye lango la USMA katika dakika zote 90 lakini zaidi kwenye kipindi cha pili baada ya mabadiliko ya wachezaji aliyokuwa akiyafanya Nabi na kama kungekuwa na umakini historia mpya ingeandikwa Tanzania.
Kipa Djigui Diarra kwa mara nyingine ameendelea kudhidhirisha umahiri wake baada ya kuokoa mkwaju wa penalti iliyotolewa katika dakika ya 59 mpigaji akiwa nahodha wa USMA, Balaid Zenadine. Penalti hiyo ilitolewa baada ya Ibrahim Bacca kumchezea rafu Tumisang Orebonye.
Kwa matokeo hayo Yanga inaishia kulamba kitita cha Sh bilioni 2.3 wakati vinara USMA wao watapata Sh bilioni 4.7 ambazo anapewa bingwa wa michuano hiyo.
Matokeo hayo pia yanawapa wachezaji wa timu hiyo medali lakini pia timu hiyo ina kila sababu ya kujivunia kwa kutoa mfungaji bora wa michuano hiyo ambaye ni Fiston Mayele aliyefunga mabao saba.
Kama ambavyo Yanga walikuwa wakipigania kubeba taji la kwanza la michuano hiyo, USMA nao walikuwa na azma hiyo hiyo ambayo wameifanikisha wakati kwa Yanga imeshindikana na hivyo Juni 3, 2023 inabaki kuwa kumbukumbu kwa Yanga kufikia hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Nje ya hayo Yanga inakuwa imepoteza fursa ya kubeba mataji matatu katika msimu mmoja na sasa inabakiwa na fursa ya kubeba mataji mawili kama itafunga Azam katika mechi ya fainali ya Kombe la FA itakayopigwa Juni 12 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
USMA: Benbot, Radouani, Loucif, Alilet, Belaid, Chita, Bousseliou/Belkacemi, Merbah/Meziane, Mahious/Benkhelifa, Merili na Orebonye.
Yanga: Diarra, Djuma Shaban/Moloko, Lomalisa/Farid Mussa, Bacca, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Tuisila Kisinda/Ben Morrison, Aboubakar Salum, Mayele, Mudathir Yahya/Clement Mzize na Musonda/Aziz Ki.
Kimataifa Yanga yakwama Algeria
Yanga yakwama Algeria
Read also
