Algers, Algeria
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra ambaye ametwaa tuzo ya nyota wa mchezo katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, amesema timu yake itashiriki mashindano hayo mwakani ikiwa imara zaidi.
Yanga ilikwama kubeba taji la michuano hiyo licha ya kuichapa USM Algers bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa jana Jumamosi mjini Algers, Algeria.
Licha ya ushindi huo, Yanga imeangushwa na kanuni ya bao la ugenini baada ya kulala kwa mabao 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Diarra alinukuliwa kwenye mtandao wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) akitoa kauli hiyo na kusisitiza kwamba mwakani Yanga itakuwa imara na shauku ya ushindi ikiwa imeongezeka.
“Tutakuja tena tukiwa imara na kuhakikisha tunafanya vizuri, tuna uzoefu na wachezaji wanataka kurudi katika safari hii kwa mara nyingine,” alisema Diarra.
“Tulijitoa kwa kila kitu na kucheza kwa ubora bahati mbaya hilo halikutosha, tuliota ndoto ya taji hili kama vichaa na tulikuwa na haki ya kushinda lakini bahati haikuwa upande wetu,” alisema kipa huyo kutoka nchini Mali mara baada ya mechi hiyo.

Akizungumzia kuibuka nyota wa mchezo huo, Diarra alisema kwamba amefurahishwa na jambo hilo na kwake ni heshima na ingependeza zaidi kama angebeba na taji la michuano hiyo.
“Najisikia furaha kuwa nyota wa mchezo katika mechi ya fainali, ni heshima kwangu ila ingependeza kama ingeambatana na kombe lakini haikuwa hivyo, najivunia wachezaji wenzangu na kikosi kizima, tumepambana vizuri,” aliongeza Diarra.
Kiwango cha Diarra katika mechi hiyo kilikuwa kivutio ikiwamo kuokoa penalti katika dakika ya 59 na kuokoa michomo kadhaa ya USMA lakini pia aliongoza vyema timu yake na katika dakika za mwisho alikuwa akipanda kama kupeleka mashambulizi mbele lakini bahati haikuwa kwa Yanga.
Mchezaji mwingine ambaye ameipa Yanga heshima ni Fiston Mayele ambaye ameibuka mfungaji bora wa michuano hiyo akiwa amefikisha mabao saba wakati wachezaji wengine walipewa medali kama ilivyo ada kwa kushika nafasi ya pili.
Yanga kwa hatua iliyofikia pia imepata kitita cha Sh bilioni 2.3 wakati USMA ambao wameibuka vinara wamelamba Sh bilioni 4.7.
