Na mwandishi wetu
Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema manyanyaso ni kikwazo kikuu cha yeye kuondoka kwenye klabu hiyo lakini akasema endapo Rais wa Yanga, Hersi Said akiachia ngazi basi muda huohuo atarejea kuendelea na klabu hiyo.
Kauli hiyo pamoja na mengine aliyofunguka ameitoa leo Alhamisi kwenye mahojiano na kipindi cha Power Breakfast cha redio Clouds.
“Mashabiki wa Yanga nawapenda na nimechezea timu kwa jasho na kujitoa lakini hawajui kilichonitoa Yanga maana wanaaminishwa sivyo na mimi niliondoka kwa sababu ya manyanyaso na imefikia hatua nikasema bora niondoke niwape stahiki zao niondoke,” alisema.
Alisema Yanga ni taasisi kubwa na yeye ana mapenzi nayo ila hana ugomvi na Yanga bali tatizo lake kubwa ni Hersi ambaye anadai aliwahi kuzungumza naye kwa masaa sita lakini hakukuwa na mwafaka.
“Niliambiwa nauza mechi na baadhi ya viongozi na kuna mtu ndani ya viongozi alikuwa ananiambia lakini nikimpigia simu hapokei wala jumbe zangu hazijibu lakini baadaye wanakuja wanamdhalilisha mama yangu ambaye ni pepo yangu na kumtukana, hivi ingekuwa wewe mama yako anatukanwa ungejisikiaje?,” alihoji Fei.
Anasema mama yake ndiyo alimsihi kuvumilia kipindi anakaa miezi mitatu hadi minne bila mshahara na yeye akawa anampa pesa za matumizi na kumwambia avumilie maana mama yake ni shabiki wa Yanga.
Alisema hata kauli aliyosikika akiisema mama yake ya kuhusu kula ugali na sukari ni mapito ambayo aliyapitia kabla ya udhamini wa sasa wa GSM.
Kuhusu mkataba wa sasa, Fei alisema walizungumza kuongeza mkataba na walizungumzia mkataba wa miaka miwili lakini anashangaa amekuja kusaini mkataba wenye lugha ya Kiingereza wa miaka mitatu.
Pia alifafanua kwamba si kweli pesa ya Sh milioni 100 ya ada ya usajili aliipata kwa kipindi kifupi, kwani ilimchukua muda zaidi ya mwaka kukamilishiwa pesa hizo.

Hersi alipokuwa kwenye mahojiano na kituo hicho wiki iliyopita alieleza kuwa wao hawana tatizo na Fei, akimsifia ni kijana mwenye nidhamu na zaidi wamempa maamuzi matatu ya kurudi kutumikia mkataba wake au warejee mezani kuboresha maslahi yake au klabu inayomtaka Fei iende mezani kuzungumza na Yanga na wao wako tayari kujadili dili hilo.
Fei na Yanga wameingia kwenye mgogoro tangu Desemba, mwaka jana mchezaji huyo aliporejesha kiasi cha Sh milioni 112 ikiwa ni ada ya usajili na mishahara ya miezi mitatu akifafanua amefanya hivyo kama moja ya vipengele vyake vya kuvunja mkataba Yanga na kubaki huru.
