Budapest, Hungary
Kocha wa AS Roma, Jose Mourinho (pichani) amesema hajafanya mazungumzo na klabu yoyote na kitu pekee anachofikiria kwa sasa ni kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Europa Ligi leo Jumatano.
Roma leo itakuwa dimbani mjini Budapest, Romania katika mechi ya fainali ya Europa Ligi dhidi ya Sevilla ya Hispania lakini Mourinho amekuwa akihusishwa na mipango ya kuondoka katika klabu hiyo.
Mourinho ana mwaka mmoja katika mkataba wake na AS Roma lakini tayari ameanza kutajwa katika klabu nyingine ikiwamo klabu yake ya zamani ya Real Madrid ili achukue nafasi ya Carlo Ancelotti ambaye zipo habari kwamba anatakiwa timu ya Taifa ya Brazil.
“Kwa hakika sijafanya mazungumzo na klabu nyingine, nafikiria kuhusu kesho (leo Jumatano) na nini tunachotaka kukifanya kwa sababu tunataka kucheza,” alisema Mourinho ambaye pia amewahi kuzinoa klabu za Chelsea, Inter Milan, FC Porto, Man United na Tottenham.
Msimu uliopita Mourinho aliiongoza vyema AS Roma na kubeba taji la michuao ya Europa Conference Ligi ambalo ni taji lake la tano katika michuano ya klabu Ulaya na leo anawania taji la sita.
Mourinho ana rekodi nzuri ya kushinda michuano ya klabu Ulaya katika hatua ya fainali lakini leo anakumbana na timu yenye rekodi ya kushinda fainali sita za mwisho za michuano hiyo ilizoshiriki.
“Historia haichezi, mwenzangu (kocha wa Sevilla Jose Mendilibar) anafikiria tofauti, namheshimu, anaamini historia inawafanya Sevilla wawe na nafasi kubwa ya kushinda, naliheshimu hilo, tupo katika fainali kwa sababu tuna sifa, wana historia ambayo sisi hatuna,” alisema.
“Kwa wao kucheza fainali ya Europa ni kitu cha kawaida, kwetu sisi ni tukio la kipekee, kwa mashabiki wao kwenda kwenye mechi ya fainali ni kama vile wanaenda kwenye mechi ya ligi, kwetu sisi ni jambo lisilo sahaulika,” alisema.
“Wachezaji wa Sevilla wana uzoefu zaidi lakini sisi tumekuwa pamoja kwa miaka miwili,” aliongeza Mourinho ambaye pia anaamini timu yake ipo tayari.
