Na mwandishi wetu
Wakati kikosi cha Yanga kikitarajia kuondoka kesho Alhamisi kuelekea Algeria kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha msaidizi wa timu hiyo, Cedric Kaze amesema wapo tayari kwa vita hiyo.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Jumapili iliyopita Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga ilifungwa mabao 2-1 hivyo ili kubeba taji hilo inalazimika kushinda kuanzia mabao 2-0.
Kaze (pichani juu) alisema kuwa wametumia vizuri siku mbili za mazoezi kuyafanyia kazi mapungufu ambayo waliyaona kwenye mchezo uliopita ambao walipoteza mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.
“Tunatambua uzito wa mchezo wa marudiano kwa kuwa tutakuwa ugenini, kitu kizuri ni kwamba tunakwenda tukiwa tunawajua vizuri wapinzani wetu USM Alger na tumeandaa mbinu mbadala za kuwadhibiti na kupata ushindi,” alisema Kaze.
Kocha huyo alisema wachezaji wao wako fiti akiwemo Stephene Aziz Ki, ambaye katika mchezo wa mkondo wa kwanza alitoka kutokana na kukabiliwa na maumivu ya mguu wa kushoto.
Alisema benchi la ufundi pamoja na wachezaji wote kwa pamoja wameupa uzito mkubwa mchezo huo lengo ni kuhakikisha wanacheza kwa umakini na kupata ushindi ambao utawapa ubingwa na kurudi na kombe hilo Tanzania.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu inatarajiwa kuchezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Julai 5, 1962, mjini Algiers kuanzia saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Kimataifa Kaze adai Yanga ipo tayari
Kaze adai Yanga ipo tayari
Read also