Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm ameuomba uongozi wa timu hiyo kuhakikisha unawabakisha kikosini wachezaji wake nyota ili kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao.
Singida BS huenda ikawa miongoni mwa timu nne zitakazopeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kama itamaliza ligi kwenye nafasi nne za juu.
Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi, alieleza kuwa amekuwa na hofu baada ya kuona kupitia mitandao baadhi ya nyota wake akiwemo kiungo Mbrazil, Bruno Gomes na beki wa kushoto, Nickson Kibabage wakihitajika na Yanga.
“Tunatakiwa kulinda wachezaji wetu muhimu kwa ili kufikia mafanikio kama timu nyingine zinavyofanya, kama tutauza wachezaji muhimu itakuwa ngumu kufika tulipokusudia halafu baadaye lawama zinarudi kwa kocha,” alisema Pluijm.
Kocha huyo alieleza kuwa anatambua kuwa ukiitoa Yanga, ambayo tayari inahusishwa kuhitaji wachezaji wao zipo timu nyingine nyingi za ndani na nje ya Tanzania zinawatamani wachezaji wao, hivyo ni vyema uongozi ukafunga milango kwa kukataa ofa zao.
Alisema anajua mpira ni biashara lakini kitu cha msingi kwa sasa wanapaswa kufikia malengo ambayo wamekusudia kuyafikia msimu ujao kwenye michuano yote watakayoshiriki.
