Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amemsamehe ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe huku akidai kwamba anaamini Yanga ina uwezo wa kubeba Kombe la Shirikisho Afrika iwapo itajipanga vizuri.
Yanga itakuwa ugenini Algeria Juni 3 kucheza mechi ya pili ya nusu fainali ambapo Mgunda amesema kwamba timu hiyo ina uwezo wa kushinda mechi hiyo na kubeba taji licha ya kulala kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mgunda ambaye ni kocha na mchezaji wa zamani wa Coastal Union amesema wanachotakiwa kufanya Yanga ni kuandaa mpango mkakati utakaowawezesha kufunga mabao mawili ya haraka ili kuwavuruga wenyeji wao na kuufanya mchezo kuwa rahisi.
“Bado Yanga ina nafasi ya kubeba ubingwa, naheshimu uwezo wao, naamini kuelekea mchezo wa marudiano itakuwa wameandaa mbinu mbadala itakayowapa matokeo chanya na kubeba ubingwa, wachezaji wa Yanga ni wapambanaji naamini watapambana kuipigania timu yao na taifa,” alisema Mgunda.
Akimzungumzia Kamwe Mgunda alisema hana tatizo lolote na ofisa habari huyo kwani alimuomba msamaha na yeye kama mzazi alimsamehe kama kijana wake wa kumzaa.
Mgunda alisema anajua kijana wake aliteleza na alikuwa katika harakati za kupigania mkate wake hivyo hayo yalishakwisha na anamwombea mafanikio mema katika mechi ya marudiano ya mchezo wao huo wa fainali.
“Sina tatizo na Kamwe sababu namchukulia kama kijana wangu, kizuri amegundua kosa lake na ameomba msamaha na mimi kama mzazi nimeshamsamehe na namtakia mafanikio mema kwenye kazi yake ikiwemo kuchukua ubingwa wa Afrika,” alisema Mgunda.
