Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumapili imeanza vibaya mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa mabao 2-1 na USM Alger mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Wageni USMA waliandika bao la kwanza katika dakika ya 32 lililofungwa na Aiman Mahious ambaye aliwazidi ujanja mabeki wa Yanga na kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Brahima.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya Dickson Job kumchezea rafu Brahima ambaye kwa umakini alipiga mpira wa juu ambao Mahious aliutumia kuipatia USMA bao lililodumu kipindi chote cha kwanza.
Dakika ya 84, mashabiki wa Yanga wakiwa wamekata tamaa, Fiston Mayele aliwainua vitini na kuamsha upya matumaini ya mashabiki hao alipoifungia timu yake bao la kusawazisha.
Mayele alifunga bao hilo kwa mpira ulioanzia kwa Benard Morisson aliyeingia badala ya Tuisila Kisinda, Morrison aliudokoa mpira wa juu na kumkuta Mudathir aliyemuunganishia Mayele pasi ya kichwa na Mayele akautuliza kabla ya kufumua shuti lililokwenda wavuni.
Kwa Mayele hilo linakuwa bao lake la saba kwenye michuano hiyo na hivyo kuendeleza dhamira yake ya kutaka kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo huku akiwa ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu NBC na mabao yake 16.
Furaha ya mashabiki wa Yanga hata hivyo ilidumu dakika mbili tu baada ya USMA kuongeza bao la pili lililofungwa na Meril ambaye akiwa karibu na lango la Yanga aliunganishiwa pasi na kwa utulivu akaujaza mpira wavuni kwa shuti lililoonekana kumpoteza maboya kipa wa Yanga, Djigui Diarra.
Yanga pamoja na kipigo hicho lakini ilionyesha uhai tangu mwanzoni wa mchezo, mfano dakika ya 22, Mayele aliambaa na mpira kulia mwa lango la USMA na kufumua shuti la chinichini ambalo lilimpita kipa wa USMA, Benbot lakini baada ya kumpita kipa huyo wachezaji wa Yanga walishindwa kumalizia kwa kuujaza wavuni.

Dakika ya 49 tena kona fupi ya Aziz Ki ilimkuta Kisinda ambaye aliunganisha mpira vizuri katika lango la USMA lakini mpira huo uliwashinda, Mayele na Mwamnyeto na kutokuwa na madhara yoyote.
Aziz Ki ambaye baadaye alitolewa na nafasi yake kuingia Salum Aboubakar, dakika ya 64 alipiga kiufundi mpira wa adhabu uliotokana na rafu aliyochezewa Mudathir lakini umahiri wa kipa Benbot ulikuwa kikwazo na kuinyima Yanga bao.
Kwa matokeo hayo, Yanga inakuwa imezikosa Sh 20 milioni ambazo Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuzitoa kwa kila bao la timu hiyo lakini kwa sharti bao hilo liwe limeipa timu ushindi.
Yanga sasa inasubiri kurudiana na USMA ugenini Algeria, mechi itakayopigwa Juni 3 na ikiweza kupindua meza itabeba kombe na kulamba kitita cha Sh 4.7 bilioni, matokeo yakikuwa mabaya timu hiyo italamba Sh 2.3 bilioni. Lolote linawezekana, bado kuna dakika nyingine 90 za kutafuta matokeo.
