Manchester, England
Straika wa Man City, Erling Haaland leo Jumamosi ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu akiwa pia ameshinda tuzo ya mchezaji bora kijana na kuwa mchezaji wa kwanza kubeba tuzo zote mbili kwa msimu mmoja.
Haaland (pichani) mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao 36 katika mechi 35 msimu huu ambayo pia yameiwezesha Man City kubeba taji la Ligi Kuu England (EPL) kwa mara ya tatu mfululizo.
Kwa idadi hiyo ya mabao anakuwa amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mastraika wa zamani Andy Cole wa Man United na Alan Shearer wa Newcastle waliofikisha mabao 34 katika msimu mmoja takriban miaka 30 iliyopita.
Haaland ambaye katika michuano yote ana mabao 52 msimu huu, bado ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao kesho Jumapili, Man City itakapocheza mechi yake ya mwisho ya EPL dhidi ya Brentford.
Tuzo hizo kwa Haaland zimetolewa baada ya kura zilizopigwa na umma na nyingine kupigwa na manahodha wa timu 20 za EPL na nyingine zikipigwa na wataalamu wa soka.
“Nimepata heshima kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo zote mbili katika msimu mmoja,” alisema Haaland.
“Imekuwa msimu mzuri katika ligi kuu, na kubeba taji wiki iliyopita mbele ya mashabiki wetu kwenye uwanja wa Etihad ni tukio la kipekee kwangu,” aliongeza Haaland.
Mbali na tuzo hiyo, Haaland pia alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya Chama cha Waandishi wa Habari za Soka baada ya kuweka rekodi kwa kupata asilimia 82 ya kura zilizopigwa.
