Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Minziro amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kuifikisha timu hiyo hapo ilipo licha ya changamoto nyingi walizopitia msimu huu.
Geita inashikilia nafasi ya sita kwa pointi 37 ikipambana kumaliza ndani ya tano bora katika michezo miwili iliyosalia kabla ya kufungwa pazia la Ligi Kuu NBC msimu wa 2022-23.
Minziro (pichani juu) alifafanua kwamba haikuwa rahisi kwa timu hiyo kuendelea kupambana na kufika hapo licha ya kuondokewa na wachezaji wao wengi waliokuwa wakiunda kikosi cha kwanza cha timu hiyo ilioyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu huu.
“Kama ilivyoonekana wachezaji wengi waliondoka kwenye dirisha dogo la usajili na wengi walikuwa ni kikosi cha kwanza lakini wachezaji waliobaki walipambana, tukawa pamoja na tumefika hapa nawapongeza sana.
“Bado tunajipanga kuhakikisha tunamaliza ligi ndani ya tano bora, tunapishana pointi mbili na Namungo walio nafasi ya tano, hivyo bado tuna nafasi na wachezaji wapambanaji ninao pia,” alisema Minziro.
Miongoni mwa nyota walioihama timu hiyo katika dirisha dogo ni Saido Ntbazonkiza aliyeenda Simba, Yahya Mbegu aliyetua Ihefu, Kevin Nashon na Yusuf Kagoma waliotimkia Singida BS na George Mpole aliyesajiliwa FC Lupopo ya DR Congo.
