Na mwandishi wetu
Uongozi wa Simba upo katika mchakato wa kumsaka mtaalamu wa kubaini vipaji vya wachezaji (scout), na kuwasajili kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwa mafanikio kuanzia msimu ujao wa 2023-24.
Inaelezwa kuwa kufanya vibaya kwa timu hiyo katika misimu miwili iliyopita kumetokana na usajili mbovu ambao haukuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake, hivyo sasa wamemua kupanua wigo wa benchi lao la ufundi kwa kuleta wataalam wapya.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa jopo la viongozi wa juu wa timu hiyo wamekutana hivi karibuni kujadili namna ya kupata wataalamu hao ili wasaidie kazi hiyo katika dirisha lijalo la usajili.
“Msimu ujao tumedhamiria kuja kivingine kabisa hasa katika mafanikio ya ndani ya uwanja ndio maana tumeangalia tulipoangukia ambako ni kwenye ubora wa wachezaji ndio maana uongozi umepanga kupanua benchi la ufundi kwa kuleta wataalamu wa kusajili wachezaji ambao watairudisha Simba kwenye ubora,” alisema Ally.
Alisema wanashukuru viongozi wa Simba ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi ya kuleta wachezaji ambao wamewapa mafanikio mpaka sasa lakini kwa kuzingatia mabadiliko ya soka duniani inawapasa kufanya hivyo ili kupata maendeleo stahiki.
