Na mwandishi wetu
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Wizara ya Utamaduni na wadau wa michezo wamechangia tiketi 10,000 kwa mashabiki wa Yanga kwa ajili ya mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hatua hiyo ina lengo la kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha kujitoa kuhakikisha Kombe la Shirikisho Afrika linakuja Tanzania.
Yanga inatarajia kuumana na USMA Alger katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo utakaopigwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza leo Jumatano Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha (pichani), alisema Rais Samia amekuwa chachu kubwa kwenye sekta ya michezo hususani kwa klabu hizi mbili.
“Ukiacha hilo Rais Samia ametoa maelekezo kwa Wizara, Baraza la Michezo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya kazi pamoja na Yanga kuelekea mchezo huu na kuzingatia maagizo hayo muhimu.
“Tayari tumekaa vikao kadhaa na kujadiliana masuala mbalimbali ambayo kwa upande wa klabu wanahitaji msaada, tumeyapokea na tunayafanyia kazi, lengo letu ni kuhakikisha timu hii inafanya vizuri,” alisema Msitha.
Alisema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia njia kwa kutoa pesa, ndege na tiketi 5,000 kwa ajili ya mashabiki kuingia uwanjani katika mchezo huo hivyo na wao wameunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia tiketi 10,000.
