Na mwandishi wetu
Simba kesho Jumatano inatarajia kurejea kuanza mazoezi ya kujipanga kwa ajili ya mechi zao mbili za mwisho za Ligi Kuu NBC baada ya kuwa na mapumziko ya siku mbili.
Wekundu hao juzi walitangaza kupumzika kufanya mazoezi baada ya kupelekwa mbele kwa mechi yao inayofuata dhidi ya Polisi Tanzania, awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Mei 24 kabla ya kusogezwa mpaka Juni 6, mwaka huu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kupangua ratiba hiyo kwa ajili ya kuipa nafasi Yanga kujipanga vyema kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Mei 28 na Juni 3, mwaka huu.
“Kutokana na mchezo ujao wa ligi kuu kusogezwa mbele hadi Juni 6, timu ilikwenda mapumziko na kesho itarejea mazoezini chini ya kocha Robertinho (Roberto Oliveira) kwa ajili ya kuhakikisha tunamaliza kwa heshima mechi hizi mbili,” alisema Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally.
Alisema kwa sasa wameweka nguvu kubwa kuelekea kumaliza mechi zao hizo kwa heshima ambazo ni dhidi ya Polisi na Coastal Union, kisha watageukia kwenye usajili, kurekebisha timu hiyo ili iwape raha zaidi mashabiki wao msimu ujao baada ya kuteleza msimu huu.
Simba ambayo imeukosa ubingwa wa ligi kwa msimu wa pili mfululizo itamaliza ratiba yake msimu huu kwa michezo hiyo watayakayokuwa nyumbani, ikitarajia kupigwa Azam Complex, Dar es Salaam.
