Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga amesema anayatumia mapumziko ya Ligi Kuu NBC kukifanyia marekebisho kikosi chake ili kuhakikisha anakusanya pointi sita na kujiondoa chini ya msimamo wa ligi hiyo.
Mtibwa inayoshika nafasi ya 14 baada ya michezo 28 na kujikusanyia pointi 29 inatarajiwa kuwakabili Kagera Sugar Juni 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro.
Wakata Miwa hao wanatarajia kumaliza msimu huu wa 2022-23 Juni 9, kwa kuwaalika Geita Gold kwenye Uwanja wa Manungu Complex.
Mayanga (pichani juu) alisema baada ya ligi kusogezwa mbele anaendelea kuyafanyia kazi mapungufu ya kikosi na kuweka mikakati ya kuhakikisha wanakusanya pointi zote zilizosalia kabla ya kufungwa rasmi kwa ligi msimu huu.
“Bado hatuko kwenye eneo zuri kwenye msimamo, tunahitaji ushindi zaidi kwenye michezo ijayo tukianza na ule wa Kagera Sugar ambao naamini utakuwa mgumu maana tumetoka kupoteza mechi iliyopita.
“Lakini pia tutamaliza msimu kwa kucheza na Geita Gold, kwenye uwanja wetu wa nyumbani hivyo hatupaswi kufanya makosa katika mchezo huo pia,” alisema Mayanga.
