Milan, Italia
Juventus imenyang’anya pointi 10 katika Ligi ya Serie A kwa makosa ya kwenda kinyume na taratibu za usajili na hivyo kupoteza nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Januari mwaka huu, klabu hiyo ilinyang’anya pointi 15 kwa kosa hilo lakini mwezi uliopita, uamuzi huo ulibatilishwa na mahakama ya juu ya michezo nchini humo baada ya Juve kukata rufaa.
Baada ya shauri hilo kupitiwa upya hatimaye uamuzi mpya wa kuinyang’anya Juve pointi 10 ulifikiwa jana Jumatatu na mahakama hiyo saa kadhaa kabla ya timu hiyo kufungwa mabao 4-1 na Empoli.
Kwa uamuzi huo, Juve sasa inashuka hadi nafasi ya saba kwenye Serie A na kuitoa rasmi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo ni michuano mikubwa na yenye hadhi kwa ngazi ya klabu.
“Ni hali mbaya imetokea, uamuzi umekuja dakika 10 kabla ya mechi kumalizika,” alisema kocha wa Juve, Massimiliano Allegri.
Katika maombi yake ya kutaka uamuzi huo upitiwe upya, Juve pia ilitaka viongozi wake waliofungiwa wafutiwe makosa yao akiwamo aliyekuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Pavel Nedved ambaye yeye na wenzake awali walifungiwa miezi minane kujihusisha na soka lakini sasa wamefutiwa adhabu.
Maofisa wengine wa klabu hiyo waliofutiwa adhabu ni Assia Grazioli Venier, Caitlin Mary Hughes, Paolo Garimberti, Enrico Vellano, Daniela Marilungo na Francesco Roncaglio lakini mwenyekiti wa zamani, Andrea Agnelli, ofisa mtendaji mkuu Maurizio Arrivabene pamoja na wakurugenzi wa michezo, Federico Cherubini na Fabio Paratici wataendelea kutumikia adhabu.
Baada ya adhabu ya kunyang’anywa pointi 10 kutolewa taarifa ya Juve iliyokuja baadaye ilieleza kuwa viongozi wataijadili taarifa hiyo baada ya kuisoma na kisha kuangalia taratibu za kukata rufaa.
Klabu ya Napoli tayari imetangazwa bingwa wa Serie A msimu huu wakati Juve kabla ya uamuzi wa kunya’anywa pointi 10 kufikiwa ilikuwa nafasi ya pili ikiachwa kwa tofauti ya pointi 17.
Uamuzi wa kuinyang’anya Juve pointi unatokana na uchunguzi wa sakata la miaka miwili kati ya 2019 hadi 2021 ambapo klabu hiyo inadaiwa kucheza michezo michafu katika usajili kwa kuficha baadhi ya nyaraka ikidaiwa kujipatia Euro 60 milioni.
