Na mwandishi wetu
Nahodha wa Simba, John Bocco (pichani) anatarajia kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia timu hiyo baada ya mkataba wa sasa kueleka ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu alieleza kuwa uongozi pamoja na benchi la ufundi umekusudia kumuongeza mkataba mchezaji huyo kutokana na mchango wake ndani ya Simba.
“Ni mchezaji mwenye mchango mkubwa na nidhamu ya hali ya juu ndani ya timu ingawa majeraha yamekuwa yakimuandama mara kwa mara lakini tunaamini ni mtu sahihi,” alisema Rweyemamu.
Meneja huyo alieleza kuwa Simba imenufaika na Bocco kwa kiwango kikubwa ikiwemo kubeba mataji mbalimbali katika misimu minne iliyopita huko nyuma ambapo mchezaji huyo mchango wake wa mabao ulikuwa mkubwa.
Alisema pamoja na mikakati waliyokuwa nayo ya kufanya usajili wa nguvu kwa ajili ya kukiboresha kikosi chao msimu ujao, pia wanaamini uwepo wa mkongwe huyo utakuwa na mchango kwenye timu yao.
Alisema uzoefu wake kwenye ligi kuu pamoja na hamasa anayotoa kwa wachezaji wenzake hasa vijana ndivyo vilivyowashawishi kumbakisha mshambuliaji huyo kwenye kikosi chao cha msimu ujao.
Bocco alijiunga na Simba misimu mitano iliyopita akitokea Azam na kuisaidia timu hiyo kubeba mataji manne ya ligi kuu, mawili ya Kombe la FA (ASFC) na robo fainali nne za michuano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
