London, England
Sasa ni rasmi Man City ndio vinara wa Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2022-23 baada ya Arsenal kulala kwa 1-0 mbele ya Nottingham Forest leo Jumamosi.
Ikiwa imebakia mechi moja katika ligi hiyo, Man City inaongoza kwa pointi nne ikifuatiwa na Arsenal inayoshika nafasi ya pili lakini imebakiwa na mechi moja na hivyo haiwezi kufikia Man City.
Bao pekee lililoizamisha Arsenal katika mechi hiyo ilifungwa na Taiwo Awoniyi katika dakika ya 19 na hivyo kuwa faida kubwa kwa Man City ambayo imetwaa taji la EPL kiulaini.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa timu hiyo kubeba taji hilo lakini kubwa zaidi ni kwamba sasa imefufua zaidi mafumaini ya kubeba mataji matatu msimu huu.
Tayari imeshabeba taji la kwanza, imefuzu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikisubiri kuumana na Inter Milan lakini pia inasubiri kucheza mechi ya fainali ya Kombe la FA dhidi ya Man United.
Mechi na Man United itapigwa Juni 3 kwenye dimba la Wembley wakati ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itapigwa Juni 10 mjini Istanbul, Uturuki ambapo Man City itakuwa ikiwania kulibeba taji hilo kwa mara ya kwanza.
Kocha wa Man City Pep Guardiola amenukuliwa hivi karibuni akisema kwamba wachezaji wake wana haki ya kupiga hesabu za mataji matatu msimu huu mara baada ya kufuzu hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ni Man United pekee iliyoweza kumaliza msimu na mataji matatu, ilifanya hivyo msimu wa 1998-99 wakati ikinolewa na Sir Alex Ferguson na sasa anasubiriwa Pep kama ataiweza rekodi hiyo.
Matokeo ya mechi za EPL leo Jumamosi…
Tottenham 1-3 Brentford
Bournemouth 0-1 Man Utd
Fulham 2-2 Crystal Palace
Liverpool 1-1 Aston Villa
Wolves 1-1 Everton
Nottm Forest 1-0 Arsenal
Kimataifa Man City baba lao England
Man City baba lao England
Read also