Na mwandishi wetu
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema mipango iliyopo mbele yao ni kuhakikisha wanashinda michezo miwili iliyobaki kwenye Ligi Kuu NBC kisha waanze mchakato wa kuijenga timu.
Simba tayari imeanza mazoezi kujiandaa na michezo hiyo ya kuhitimisha ligi msimu huu ambapo watacheza dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, michezo yote wakiwa nyumbani.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Robertinho alisema wameanza mazoezi ya kujiweka imara na tayari kwa michezo hiyo ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya maandalizi ya Africa Super League.
“Tunajiandaa vizuri kwa michezo yetu miwili ya ligi kisha tutaelekeza nguvu katika michuano ya Africa Super League itakayochezwa baadaye, lengo letu baada ya ligi ni kuijenga timu kwa michuano hiyo mikubwa na kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema.
Simba inataka kumaliza kwa heshima baada ya kukosa mataji msimu huu kufuatia mtani wake wa jadi, Yanga kuchukua taji la Ligi Kuu NBC huku Robertinho akisema wao ni timu kubwa lazima washinde michezo yote iliyobaki.
Pia, alizungumzia tetesi za kutaka kuondoka kwa wachezaji Peter Banda na Pape Sakho akisema bado wana mipango nao kwa kuwa ni vijana wadogo na hazina kubwa kwa timu hiyo hapo baadaye.
“Nina furaha kuhusu wachezaji wadogo wawili Banda na Sakho kwa sababu wapo kwa ajili ya klabu na inawategemea kama vijana wadogo watakaoisaidia timu baadaye,” alisema Robertinho aliyetua Simba katikati ya msimu huu akitokea Vipers ya Uganda.