Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Prisons, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema kasi waliyonayo sasa ya kushinda mechi mfululizo ndio watakayoanza nayo msimu ujao wa Ligi Kuu NBC.
Prisons ambayo ilikuwa ikiyumba kabla ya kuanza kushinda mechi zake na kushika nafasi ya nane kwa pointi 34 baada ya kuweka rekodi ya kushinda mechi nne mfululizo.
Akizungumza na GreenSports, Bares aliyeshinda tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Aprili alisema Prisons ni timu kongwe nchini na wanahitaji kufanya vizuri hivyo watahakikisha kasi wanayomaliza nayo ligi sasa ndio watakayoanza nayo msimu ujao na kuwa tishio.
“Wengi wanaifahamu Prisons ni timu kongwe Tanzania, lakini nafikiri ni upepo mbaya tu ulimpitia mtangulizi wangu (Patrick Odhiambo) na nimeyaona machache nimeyafanyia kazi, vijana wamebadilika, tunataka hiyo kasi tunayomaliza nayo tuanze nayo msimu ujao,” alisema Bares.
Bares aliyeanza kuinoa Prisons Februari, mwaka huu akitokea Mlandege ya Zanzibar alisema Ligi Kuu NBC imeonesha kuimarika ndio maana kuna timu nyingi zinapata shida kwenye mabadiliko hayo ya ugumu wa mechi lakini anaamini ataitengeneza Prisons katika ushindani huo msimu ujao.
