Na mwandishi wetu
Rais wa Yanga, Hersi Said amesema kwa mafanikio ambayo timu hiyo imeyapata msimu huu, itakuwa rahisi kwao kumpata mchezaji yeyote mzuri wanayemuhitaji kuelekea msimu ujao.
Hiyo ni baada ya Yanga kuutetetea ubingwa wa Ligi Kuu NBC Jumamosi iliyopita huku Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS) likiitaja timu hiyo kushika nafasi ya tisa kwa ubora Afrika ikipanda kwa nafasi 10 huku ikiwa nafasi ya 104 duniani.
Hersi amesema hayo hayakufanikiwa kwa wepesi kwani walitumia muda kuijenga timu hiyo na yeye amehusika kwa asilimia zote kusajili wachezaji walionao sasa takriban misimu mitatu iliyopita na kuwa sababu ya kupeleka furaha Jangwani hivyo anafahamu angalau kipindi hiki mambo yamekuwa mepesi.
“Nitoe mfano wa Aziz Ki (Stephane), nilikwenda Morocco wakati wanacheza na RS Berkane kwa ajili ya kuzungumza naye kabla ya kwenda Ivory Coast kuzungumza na mama yake,” alisema Hersi.
“Haikuwa rahisi maana mameneja au wazazi wanataka kuona tuko makini kwa kiasi gani na sasa wameona tulichokifanya na hivyo ni rahisi kumleta mchezaji yeyote hata kama ni wa Afrika Kusini,” alisema Hersi.
Alisema miaka miwili ya awali akiwa mwenyekiti wa mabadiliko ya uendeshaji kabla ya kuwa rais, Yanga ilikuwa chini mno kabla ya kuanza kuijenga upya kuanzia makipa, mabeki, viungo na washambuliaji waliopo na kwamba haikuwa rahisi kwa wakati huo.
“Mwaka wa tatu ambao ni msimu uliopita tukawa mabingwa kwa ajili ya usajili mzuri na sasa tumekuwa tena mabingwa, si kwamba ni suala ambalo limekuja tu, ni kutokana na kikosi cha wachezaji 28 ambao ni kikosi kizima, nimesajili karibu misimu mitatu iliyopita ingawa haikuwa rahisi,” alisema Hersi.
Ukiachana na ligi, Yanga tayari imetwaa Ngao ya Jamii, ikipambana kuuteteta ubingwa wa Kombe la FA (ASFC) wakiwa hatua ya nusu fainali na kesho Jumatano wanatarajia kuumana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo wa kwanza, Yanga ikiwa mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
