Na mwandishi wetu
Uongozi wa klabu ya Simba umesema kuwa haujapata taarifa yoyote kutoka klabu ya TP Mazembe ya DR Congo ya kutakiwa kwa mshambuliaji Jean Baleke.
Baleke alijiunga na Simba kwa mkopo wa miaka miwili akitokea Mazembe na tangu amejiunga na timu hiyo amekuwa na kiwango kizuri akiwafungia Wekundu hao mabao 11, kati ya hayo saba ameyafunga kwenye ligi na manne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo juzi Alhamisi kulizuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Mazembe imepokea ofa ya kutakiwa kwa mshambuliaji huyo na moja ya timu za Ulaya na kwamba taarifa hiyo ilieleza kuwa Baleke mwenyewe yuko tayari kwa ofa hiyo.
Ofisa Habari wa Simba Ahmed Ally ameiambia GreenSports kuwa hawajapata taarifa zozote kutoka Mazembe wanaommiliki mchezaji huyo juu ya kutakiwa kwake na moja ya klabu za Ulaya.
Ally pia alisema kwamba Simba hawako tayari kumuachia mchezaji huyo kwani wana mkataba nae wa mkopo wa miaka miwili.
“Baada ya kusikia habari hiyo nikawauliza mtendaji mkuu (Imani Kajula) na mwanasheria wa klabu, wote wamenithibitishia hakuna taarifa za ofa ya Baleke kutoka Mazembe. Niseme Baleke bado tuna mkataba nae wa mkopo wa miaka miwili,” alisema Ally.
“Ndio maana huwa tunasema ni mchezaji wetu kwa sababu tunaye kwa muda mrefu na ikitokea Mazembe wanamuhitaji kabla ya muda huo kuna taratibu nyingi za kufuatwa sababu mkopo wake ulitugharimu fedha nyingi kumpata,” alisema Ally.
Alisema mchezaji huyo aliyetua Simba Januari, mwaka huu hata wao wana mipango naye ya msimu ujao ndiyo maana yupo hapo kwa muda mrefu hivyo mashabiki na wadau wa timu hiyo wapunguze presha.
Soka Simba haina taarifa Baleke kutakiwa Mazembe
Simba haina taarifa Baleke kutakiwa Mazembe
Read also
