Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa KMC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema hawaihofii timu yoyote na watahakikisha mechi mbili zilizosalia wanazitumia sawasawa kusalia Ligi Kuu NBC msimu ujao.
Julio ameyasema hayo baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Big Stars na kufikisha pointi 29 zilizowatoa nafasi ya 14 mpaka ya 12.
Hiyo ni mechi ya pili kwa Julio tangu akabidhiwe timu hiyo wiki nne zilizopita akirithi mikoba ya Thierry Hitimana, mechi ya kwanza alipoteza dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0 kabla ya kuifunga Singida Big kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
“Nimewaeleza kwamba haijaisha mpaka iishe, tulifungwa na Dodoma, tumeshinda na Singida, bado tuna mechi mbili mkononi dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons ambao wapo kama sisi, kwa hiyo tutahakikisha tunapambana tuone nani aliyejipanga vizuri na kupata ushindi.
“Hatuna mtu wa kumuogopa, huu ni mpira na kwenye mpira kikubwa ni kujipanga na kushindana, wapo kwao na sisi tutatoka kwetu kwenda kushindana, atakayekuwa na bahati ambaye naamini ni mimi tutashinda mechi,” alisema Julio.
Mbeya City iliyo nafasi ya 14 na pointi 27 inapambana isishuke daraja ikiwa imebakiza mechi tatu kama Prisons wanaoshika nafasi ya tisa kwa pointi 31 lakini wakihitaji ushindi waepuke kwenda chini na kucheza mechi za mtoano kuwania kusalia kwenye ligi msimu ujao.
