Na mwandishi wetu
Hatimaye leo Jumamosi Yanga imetawazwa rasmi vinara wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2022-23 baada ya kuilaza Dodoma Jiji mabao 4-2 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 74 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika ligi hiyo huku ikiwa na michezo miwili kabla ya kukamilisha mechi zake zote 30 katika ligi hiyo yenye timu 16.
Yanga ambayo inalibeba taji hilo kwa mara ya pili mfululizo baada ya kulibeba msimu uliopita, pia inakuwa imefuta matumaini ya mahasimu wao Simba ambao wana pointi 67 na walikuwa wakisubiri kwa hamu Yanga iteleze katika mechi zilizobaki.
Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 38 lililofungwa na Kennedy Musonda kwa shuti kali baada ya kuinasa pasi ya Stephanie Aziz Ki ambaye naye aliunganishiwa mpira na Benard Morisson.
Dodoma hata hivyo hawakuonekana kuyumba na katika dakika ya 58 walisawazisha bao hilo mfungaji akiwa ni Collins Opare ambaye aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Salmin Hoza.
Dakika nane baadaye Dodoma Jiji waliandika bao la pili lililofungwa na Seif Rashid ambaye aliupiga kiufundi mpira wa juu akitokea upande wa kushoto wa lango la Yanga na kumuacha kipa Metacha Mnata akiuangalia mpira unavyojaa wavuni asiamini kilichotokea.
Mudathir Yahya aliyeingia kuchukua nafasi ya Aziz Ki aliwainua vitini mashabiki wa Yanga walionekana kuanza kukata tamaa baada ya kusawazisha bao hilo dakika ya 70 akiitumia pasi ya Clement Mzize aliyeingia badala ya Benard Morisson.
Bao hilo liliwaamsha wachezaji wa Yanga na kuanza kulisakama lango la Dodoma Jiji ambao walikuwa na kazi ya kujihami na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza na wakati mwingine wakitumia mbinu ya kuchelewesha muda.
Katika matukio yanayoaminika ya kuchelewesha muda, Anderson Kimweri alipewa kadi ya njano kwa kuchelewesha mpira wa kurusha wakati kipa wake, Aron Kalambo naye alipewa kadi kama hiyo kwa kosa hilo hilo.
Juhudi za Yanga zilizaa matunda dakika ya 87 walipoandika bao la tatu lililofungwa na Farid Mussa, bao hilo lilitokana na kona mbili mfululizo ambazo zote zilichongwa na Djuma Shaban, baada ya kona ya kwanza kuokolewa, ya pili ikazaa bao.
Katika dakika nne za nyongeza Yanga iliandika bao la nne ambalo lilifungwa na Mudathir na ingeweza kupata bao la tano katika muda huo baada ya Fiston Mayele kumpunguza beki mmoja wa Dodoma Jiji lakini akiwa karibu kabisa na lango la Dodoma Jiji alishindwa kuujaza mpira wavuni.
Katika muda huo huo Dodoma Jiji ilipata pigo baada ya mchezaji wake, Mbwana Kibuta kupewa kadi nyekundu.
Soka Hatimaye…
Hatimaye…
Read also
