Na mwandishi wetu
Simba kesho Ijumaa inatarajia kushuka dimbani katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuvaana na Ruvu Shooting ikiwa ni mchezo wa raundi ya 28 wa Ligi Kuu NBC iliyoko ukingoni.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo na kuharibu hesabu zao za kuupigania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Timu hizo zinakutana zikiwa katika nafasi tofauti kwenye msimamo, Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 64 wakati Ruvu Shooting inaburuza mkia kwa pointi 20 na baada ya mchezo huo timu zote zitabakiwa na mechi mbili kila moja kabla ya msimu kuisha.
Kuelekea mchezo huo, kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda amesema maandalizi yao yanakwenda vizuri na wachezaji wake wapo katika hali nzuri kuwakabili Ruvu.
Mgunda alisema mchezaji atakayeukosa mchezo huo ni kipa Aishi Manula anayeuguza maumivu ya nyonga lakini waliobaki wapo katika hali nzuri na lengo lao ni kushinda mchezo huo ili kupoza machungu ya mashabiki wao.
“Tupo tayari kwa mchezo, wachezaji wangu wote wapo sawa kimbinu na hata kiakili, naamini utakuwa mchezo wa ushindani kutokana na Ruvu Shooting kuhitaji ushindi ili kujinasua na janga la kushuka daraja,” alisema Mgunda.
Kocha Mkuu wa Ruvu, Mbwana Makata alisema wamejiandaa kuikabili Simba, ingawa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa timu wanayokwenda kukutana nayo.
“Nikiri tu huu ni mchezo mgumu sana kwetu sababu tunakutana na timu bora kuliko tulivyo sisi na mbaya zaidi wametoka kujeruhiwa pamoja na yote tutapambana kuona wapi tutaishia lakini mambo ni magumu kwetu,” alisema Makata.
Kocha huyo alisema hakuna mchezaji atakayekosa kwenye mchezo huo kutokana na kadi au majeruhi hivyo pamoja na ugumu wa mchezo lakini wamedhamiria kupambana ili kupata ushindi.
