Na mwandishi wetu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwenye mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga ilipata ushindi huo jana Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na sasa inasubiri mechi ya marudiano itakayopigwa Afrika Kusini Mei 17, mwaka huu ikihitaji sare yoyote au kutopoteza kwa zaidi ya bao 1-0 ili kutinga fainali.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Samia pia aliitaka Yanga kuendelea kuiheshimisha nchi kwa kujipanga kikamilifu kuelekea mechi inayofuata, akisisitiza kuendelea kuwaunga mkono kwa hamasa ya fedha anazotoa.
“Hongereni Yanga kwa ushindi katika mchezo wenu wa raundi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Nawatakia maandalizi mema kwa mchezo wenu wa raundi ya pili, muendelee kuiheshimisha nchi yetu. Hamasa yangu inaendelea,” aliandika Rais Samia.
Huo umekuwa mwendelezo wa Rais Samia kuipongeza Yanga kama alivyofanya ilipotinga hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa kuitoa Club Africain ya Tunisia na hata ilipotinga robo fainali kwa kuitupa nje Rivers United ya Nigeria.
Mbali na pongezi hizo, Yanga imeendelea kuchota fedha za Rais Samia baada ya kukabidhiwa Sh milioni 20 na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Pindi Chana mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.
Kupitia hamasa hiyo ya fedha za Rais Samia kwa kila bao litakalofungwa kwenye michuano hiyo, Yanga sasa imechota jumla ya Sh 75 milioni baada ya Sh milioni 55 za mabao yao 11 ya awali.
Awali ahadi hiyo ilikuwa ni Sh 5,000,000 kwa kila bao litakalofungwa na Simba na Yanga kwenye michuano ya klabu Afrika kabla ya Simba kutolewa hatua ya robo fainali na kuvuna Sh milioni 55.
Baadaye, Rais Samia aliongeza fungu hilo na kufikia Sh 10 milioni kwa kila bao litakalofungwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo na sasa Yanga inaonekana kuendelea kunufaika vilivyo na hamasa hiyo.
Ikiwa ni mara ya kwanza kwa Rais Samia kuziunga mkono timu za Tanzania kwenye michuano hiyo, pia timu hizo zimeweka historia kwa mara ya kwanza zote mbili kutinga hatua ya robo fainali na sasa Yanga inakaribia kuweka rekodi mpya ya kuingia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza.
