Manchester, England
Man City imejitoa katika mbio za kuisaka saini ya kiungo wa Borussia Dortmund, Jude Bellingham badala yake imemgeukia kiungo wa Chelsea, Mateo Kovacic ikiamini anatosha kuwa mbadala wa Bellingham.
Katika siku za karibuni, Man City imekuwa ikitajwa kumuwania Bellingham ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya England lakini inaonekana kuzidiwa ujanja na Real Madrid ambayo inadaiwa kutumia nguvu nyingi kwa mchezaji huyo.
Tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia, Desemba mwaka jana, Bellingham aliyeichezea England na kuonyesha kiwango kizuri, amekuwa gumzo akihusishwa kujiunga na klabu mbalimbali barani Ulaya huku Real Madrid ikiwa mstari wa mbele.
Bellingham mwenye umri wa miaka 19 bado hajasema lolote kuhusu klabu anayotaka kujiunga nayo ingawa amekataa kuongeza mkataba na Dortmund hivyo ni wazi kwamba amedhamiria kuachana na klabu hiyo ya Ujerumani.
Kwa upande wa Kovacic ambaye alikuwa na timu ya Croatia iliyoshika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia, Desemba mwaka jana, bado hajasema lolote kuhusu ofa ya Man City japo inaaminika hatosita kuipokea changamoto hiyo mpya.
Kovacic ambaye pia amewahi kuzichezea klabu za Inter Milan na Real Madrid, inadaiwa kwamba thamani yake inafikia Pauni 22 Milioni.
Kimataifa Man City yamgeukia Kovacic
Man City yamgeukia Kovacic
Read also
