Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime (pichani) amesema anataka kushinda mechi zote tatu ili kumaliza msimu kwenye nafasi tano bora.
Kagera Sugar ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi 35 ikiwa imesaliwa na michezo mitatu kumaliza msimu huu wa 2022-23.
Maxime ameeleza kuwa anatambua ushindani uliopo katika kipindi hiki ambacho ligi inaelekea ukingoni lakini mapumziko waliyoyapata wameyatumia vizuri kujiimarisha ili kushinda mechi hizo tatu.
“Msimu wetu ulikuwa na changamoto za hapa na pale lakini kikubwa nafurahi tupo ndani ya malengo yetu mpaka sasa,” alisema Maxime aliyetua kuinoa timu hiyo katikati ya msimu akichukua nafasi ya Mkenya, Francis Baraza aliyefutwa kazi kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo.
Kocha huyo alisema baada ya msimu kumalizika anatarajia kukutana na uongozi wa timu hiyo ili kupanga mikakati ya kuisuka upya kwa ajili ya mapambano ya msimu ujao.
Mechi tatu ambazo wamebakiwa nazo Kagera Sugar kabla ya msimu kuisha ni dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa Kaitaba wiki ijayo, michezo mingine watamalizia ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Ihefu.
