Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa PSG, Lionel Messi hajafanya makubaliano yoyote na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia kama inavyodaiwa badala yake klabu mpya atakayojiunga nayo itajulikana baada ya msimu huu.
Chanzo kimoja cha habari nchini Hispania kimeeleza kuwa Messi ambaye amesimamishwa na PSG kwa wiki mbili kwa kosa la kwenda Saudi Arabia kwa masuala binafsi ya kibiashara bila ruhusa ya klabu, ameamua kutofanya uamuzi wowote kuhusu klabu atakayojiunga nayo hadi msimu huu utakapomalizika wiki chache zijazo.
Inaeleweka kwamba Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina hatoongeza mkataba na PSG baada ya mkataba wa sasa ambao unafikia ukomo baada ya msimu huu jambo ambalo linazidi kuupa nguvu mjadala wa wapi atakwenda.
Klabu ambazo zimekuwa zikitajwa kumuwania mchezaji huyo mbali na Al Hilal ya Saudia ni Inter Miami ya Marekani, Chelsea pamoja na klabu yake ya zamani ya Barca ambayo vigogo wake inadaiwa wapo tayari kumpokea mchezaji huyo kwa mikono miwili iwapo atakuwa tayari kurudi.
Kati ya klabu zote hizo, klabu ambayo inatajwa kuweka nguvu zaidi katika mbio za kumpata mchezaji huyo ni Al Hilal.
Inadaiwa matajiri wa Al Hilal wanataka mchezaji huyo aungane na ‘hasimu wake’, Cristiano Ronaldo anayeichezea klabu ya Al Nassr pia ya nchini humo, timu ambayo mpinzani wake mkuu katika soka la Saudi Arabia ni Al Hilal.
Iwapo Messi atajiunga na Al Hilal, inaaminika kwamba uwapo wake pamoja na Ronaldo utasaidia kwa kiasi kikubwa kulipa umaarufu duniani kote soka la Saudi Arabia.
Kimataifa Hatma ya Messi baada ya msimu
Hatma ya Messi baada ya msimu
Read also