Barcelona, Hispania
Nahodha, Sergio Busquets hatimaye amethibitisha kuwa ataondoka Barca baada ya msimu huu na hivyo kuhitimisha safari yake ya miaka 18 akiwa na rekodi ya kuichezea timu hiyo mechi 718 hadi sasa.
Busquets mwenye umri wa miaka 34 ambaye pia amewahi kutamba na timu ya Taifa ya Hispania, hadi sasa anashika nafasi ya tatu kati ya wachezaji walioichezea Barca mechi nyingi.
Mchezaji huyo pia anajivunia rekodi ya kubeba mataji manane ya La Liga, saba ya Copa del Rey, saba ya Spanish Super Cup na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Na ingawa haujawa uamuzi rahisi, lakini nafikiri wakati umefika, ni safari isiyosahaulika, nilikuwa wakati wote mwenye ndoto ya kucheza nikiwa na jezi ya timu hii na uwanja huu (Nou Camp), uhalisia umezidi ndoto zangu zote,” alisema Busquets.
“Imekuwa heshima kubwa, ndoto, jambo la kujifaharisha na ilimaanisha kila kitu katika kuilinda na kuiwakilisha nembo ya klabu hii kwa miaka mingi, lakini kila kitu kina mwanzo na lazima kiwe na mwisho, nataka kuwashukuru wote walionisaidia kuliwezesha hili tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho,” alisema Busquets.
Historia ya Busquets na Barca inaanzia mwaka 2005 akiwa mchezaji wa timu ya vijana na kupiga hatua hadi Barca B kabla ya kucheza kikosi cha kwanza chini ya kocha Pep Guardiola kwa mara ya kwanza mwaka 2008 katika mechi ya ligi dhidi ya Racing Santander.
Busquets ambaye alikuwa kiungo mkabaji, Desemba mwaka jana alistaafu kuichezea timu ya Taifa ya Hispania akiwa na rekodi ya kubeba Kombe la Dunia mwaka 2010 na lile la Ulaya mwaka 2012.
