London, England
Klabu ya Burnley imemsainisha mkataba mpya wa miaka mitano kocha wake, Vincent Kompany ambaye sasa atakuwa na timu hiyo hadi mwaka 2028.
Kompany ambaye ameirudisha timu hiyo kwenye Ligi Kuu England (EPL), amekuwa pia akidaiwa kutakiwa na klabu ya Chelsea iliyovutiwa na mafanikio aliyoyapata akiwa Burnley.
Katika msimu wake wa kwanza na Burnley, Kompany, beki wa zamani wa Man City, ameiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Championship akiwa na mechi kadhaa mkononi na sasa anajiandaa kuiongoza katika EPL kwa msimu wa 2023-24.
“Hakika tuna furaha, Vincent amesaini mkataba mpya, ni mtu sahihi anayefaa kwa namna ambavyo wote tunaona klabu ya soka ya Burnley inavyokwenda mbele,” alisema mwenyekiti wa klabu hiyo, Alan Pace.
“Ni kiongozi wa aina yake, ameweka malengo ya juu na anaipeleka klabu katika viwango ambavyo sote tunataka kuvifikia,” alisema.
Burnley leo Jumatatu itakuwa nyumbani kucheza mechi yake ya mwisho ya kumaliza msimu wa Champioship dhidi ya Cardiff City na baada ya mechi hiyo itakabidhiwa taji la ubingwa.
