Na mwandishi wetu
Uongozi wa Yanga unatarajia kumpa mkataba wa mwaka mmoja kipa namba mbili wa timu hiyo, Metacha Mnata.
Kipa huyo alijiunga na miamba hiyo ya Ligi Kuu NBC kwenye dirisha dogo msimu huu kwa mkataba wa mkopo wa miezi sita akitokea Singida Big Stars.
Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison ameeleza kuwa kiwango na nidhamu ya kipa huyo ndivyo vimemshawishi kocha wao, Nasrredine Nabi kupendekeza mchezaji huyo apewe mkataba mpya.
“Metacha ni kipa mzuri ameonesha nidhamu kubwa katika kipindi cha miezi sita ambayo tumekuwa naye kwenye timu lakini pia amekuwa akimpa changamoto nzuri kipa wetu, Djigui Diarra katika kupigania nafasi ya kucheza ndio maana Nabi amependekeza aongezewe mkataba,” alisema Walter.
Meneja huyo ameeleza kuwa mbali na Metacha lakini uongozi wao tayari umeanza mazungumzo na wachezaji wote ambao mikataba yao inaelekea kumalizika na kocha angependa kuendelea nao kwenye kikosi chao.
Alisema lengo lao ni kuendelea kufanya vizuri katika msimu ujao huku wakifanya usajili wa wachezaji wachache wapya kwa ajili ya kuimarisha sehemu zenye mapungufu.
Endapo kipa huyo ataongeza mkataba mpya ni wazi eneo la kipa kwenye kikosi cha Yanga litakuwa na ushindani mkubwa kutokana na uwepo pia wa Aboutwalib Mshery ambaye kwa sasa yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti kufuatia kufanyiwa upasuaji nchini Tunisia.
Soka Metacha kupewa mkataba Yanga
Metacha kupewa mkataba Yanga
Read also
