Paris, Ufaransa
Klabu ya Paris Saint Germain (PSG) ya Ufaransa imemsimamisha kwa wiki mbili mshambuliaji wake nyota Lionel Messi kwa kosa la kusafiri hadi Saudi Arabia bila ruhusa ya klabu hiyo.
Messi ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya Argentina, alifanya ziara ya Saudi Arabia baada ya kucheza kwa dakika zote 90, mechi ya PSG dhidi ya Lorient iliyopigwa Jumapili iliyopita.
Kwa adhabu hiyo, Messi ambaye hivi karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama timu hiyo, sasa hatofanya mazoezi au kucheza mechi yoyote ya PSG hadi adhabu ya wiki mbili itakapoisha.
Habari za ndani zinadai kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alienda Saudi Arabia kwa ajili ya masuala ya kibiashara akiwa ni balozi wa utalii wa nchi hiyo na inadaiwa aliomba ruhusa lakini alikataliwa.
Mkataba wa miaka miwili wa Messi na PSG unafikia ukomo majira ya kiangazi mwaka huu huku zikiwapo habari kwamba amewahi kufanya mazungumzo na klabu yake ya zamani wa Barcelona kwa nia ya kutaka kurudi katika klabu hiyo.
Machi mwaka huu makamu rais wa Barca, Rafael Yuste alikiri klabu yake kufanya mazungumzo na Messi ili arudi kwa mara nyingine katika klabu hiyo ambayo alianza kuichezea kwenye akademi tangu akiwa kijana mdogo.
Kwa adhabu aliyopewa Messi atakosekana katika mechi za Ligi 1 dhidi ya Troyes na Ajaccio huku PSG ikiwa katika nafasi nzuri ya kubeba taji la ligi hiyo ambayo imebakisha mechi tano kabla ya kumalizika.
Adhabu aliyopewa Messi maana yake ni kwamba uwezekano wa mchezaji huyo kuihama PSG baada ya msimu huu ni mkubwa ingawa haijaweza kufahamika mara moja kama atarudi Barca au ataenda Saudi Arabia kama alivyofanya Cristiano Ronaldo ingawa pia kuna klabu nchini Marekani zinazomhitaji.
Kimataifa Messi asimamishwa wiki mbili
Messi asimamishwa wiki mbili
Read also
