Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imesema kuwa Simba ina sababu ya kuwahofia kuelekea mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la FA kutokana na rekodi nzuri waliyonayo msimu huu dhidi ya wapinzani wao hao.
Simba na Azam zinatarajia kuumana Mei 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Ofisa Habari wa Azam, Hashim Ibwe alisema kuwa kikosi chao kinaendelea na maandalizi makali kwa ajili ya mchezo huo wakifahamu umuhimu wake na ingawa wana rekodi nzuri dhidi ya Simba msimu huu lakini wanaheshimu upinzani wa Wekundu hao.
“Tunafahamu hatutacheza na timu nyepesi, Simba hivi karibuni wamekuwa na wakat mzuri kwenye kalenda ya kimataifa na kwenye ligi wanashika nafasi ya pili kwahiyo sio mechi rahisi kucheza dhidi yao.
“Japokuwa sisi tuna rekodi nzuri dhidi yao, tuliwafunga mechi ya kwanza ligi kuu na tukatoka nao sare mechi ya pili, Azam ndiyo timu yenye rekodi nzuri zaidi dhidi ya simba msimu huu, hivyo Simba wana sababu ya kutuhofia na sisi pia kuwahofia, pia tunayo sababu ya kuheshimiana kwa hiyo Nangwanda itaamua,” alisema Ibwe.
Mechi ya kwanza baina ya timu hizo kwenye ligi msimu huu, Azam ilishinda kwa bao 1-0 kabla ya sare ya bao 1-1, hivyo mechi ya tatu baina yao inatarajiwa kuwa na upinzani mkali.
Ushindani wa mechi hiyo pia unachangiwa na ukweli kwamba timu hizo zitakuwa zikiwania kutwaa taji ambalo bingwa anakwenda kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
Mshindi wa mechi hiyo anatarajia kuumana na mshindi wa nusu fainali nyingine itakayozikutanisha Singida Big Stars na Yanga kwenye Uwanja wa Liti, Singida. Fainali itapigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
