Na mwandishi wetu
Jumapili imekuwa siku ya kipekee kwa mashabiki wa Yanga baada ya timu yao kufuzu nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-0 dhidi ya Rivers Utd ya Nigeria na sasa timu hiyo huenda ikaweka rekodi kwa kumaliza msimu na mataji matatu au ‘treble’.

Ushindi wa Yanga na kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika ni tukio kubwa la kihistoria kwa timu hiyo ambayo pia ipo katika nafasi nzuri ya kubeba taji la Ligi Kuu NBC kwani ndiyo inayoongoza ligi hiyo hadi sasa.
Yanga pia ipo hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam au FA na hivyo ina nafasi ya kulibeba taji hilo.
Kwa maana hiyo iwapo mambo yatakwenda kama wanavyotaka mashabiki, timu hiyo itajiwekea rekodi ya kubeba mataji matatu katika msimu huu wa 2022-23 unaoelekea ukingoni.
Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga imefuzu nusu fainali ikineemeka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya awali iliyopigwa ugenini nchini Nigeria kabla ya sare ya bila kufungana Jumapili hii jijini Dar es Salaam.
Yanga sasa inajiandaa kuumana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mechi ya nusu fainali ambapo timu hiyo itaanzia ugenini Mei 10 kabla ya kurudiana, mechi ambayo Yanga itakuwa mwenyeji.
Marumo nayo imejikatia tiketi yake ya nusu fainali baada ya kuibwaga, Pyramids kwa bao 1-0 katika mechi nyingine ya robo fainali na hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Kocha wa Yanga, Nabi katika mechi hiyo aliamua kumpanga kuanzia mwanzo mshambuliaji wake kinda, Clement Mzize ambaye hata hivyo alishindwa kuzitumia vizuri nafasi mbili kuipa Yanga mabao.
Mshambuliaji nyota wa Yanga, Fiston Mayele naye katika dakika ya 51 alishindwa kuipa Yanga bao baada ya kuunganishiwa pande na Mudathir Yahya lakini akiwa yeyey na kipa wa Rivers alishindwa kuipa Yanga bao.
Nabi pia katika mechi hiyo alimpa nafasi winga wake Benard Morrison ambaye katika siku za karibuni amekuwa akisugua benchi baada ya kuandamwa na balaa la kuwa majeruhi. Morisson aliingia kuchukua nafasi ya Aziz Ki.
Mechi hiyo hata hivyo iliingia utata baada ya kutokea adha ya kukatika umeme kwenye Uwanja wa Mkapa na hivyo mwamuzi kulazimika kusimamisha mchezo kwa takriban nusu saa kuanzia dakika ya 24.
Hili linakuwa tukio la pili la kuzimika kwa taa wakati mechi ikiendelea kwenye Uwanja wa Mkapa ambao hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa kwamba ina mpango wa kuufanyia matengenezo.
Awali tukio la taa kuzimika lilitokea kwenye uwanja huo katika mechi ya hivi karibuni ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Taifa Stars na Uganda Cranes ambapo mwamuzi alilazimika kusimamisha mchezo kwa dakika 30 kabla ya kuendelea.