Na mwandishi wetu
Licha ya jana Simba Queens kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Amani Queens lakini kocha wa Wekundu hao, Charles Lukula amekiri kuwa bado wana hali ngumu ya kutetea ubingwa wao.
Queens inashika nafasi ya pili kwa pointi 36 nyuma ya vinara JKT Queens wenye pointi 37 baada ya mechi 15. Fountain Gate Princess inashika nafasi ya tatu kwa pointi 32 baada ya mechi 14.
Lukula amesema kwamba mechi za mzunguko wa pili kuelekea mwishoni mwa ligi zimekuwa ngumu lakini anafarijika kuona wanaendelea kupata matokeo, akijivunia pia kuwa na kikosi kipana.
“Mzunguko wa pili umekuwa mgumu, wapo wanaopambana wasishuke na wanaopambana kuchukua ubingwa, kwa hiyo ligi imekuwa ngumu lakini kitu kizuri tunaendelea kupata matokeo licha ya kuwa na wachezaji tofauti tofauti kikosini katika mechi za hivi karibuni,” alisema.
Kocha huyo raia wa Uganda alifafanua kuwa kulingana na kasi ya wapinzani wao; JKT na Fountain, hawapaswi kudondosha pointi katika mechi tatu zilizobaki ili kuhakikisha wanajiweka pazuri kwenye kuupigania ubingwa huo.
“Mwaka huu bingwa atapatikana mechi moja kabla au mechi ya mwisho ya ligi, maana tumebaki watatu, Fountain na JKT na kila mechi kwetu sote ni kama fainali hivyo lazima tupambane tusipoteze alama hata moja ingawa kwenye michuano hii lengo letu Simba ni ubingwa tu si kingine,” alisema kocha huyo wa zamani wa She Corporates ya Uganda.
Soka Ubingwa mgumu Simba Queens
Ubingwa mgumu Simba Queens
Read also
