Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa KMC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amezipongeza timu za Simba na Yanga kwa hatua walizofika kwenye michuano ya klabu Afrika.
Timu hizo zimeonesha kiwango kikubwa kwenye mechi za robo fainali za michuano wanayoshiriki zikiwa tayari zimeshinda mechi zao kwanza za hatua hiyo kabla ya za marudiano zitakazopigwa Ijumaa na Jumapili hii.
Simba ikiwa nyumbani iliwachapa bao 1-0 mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika Wydad Casablanca wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rivers United ugenini kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Julio alisema timu zote zimefanya kazi kubwa, Simba wameshinda nyumbani lakini Yanga wao wamepata ushindi ugenini ambako mara ya kwanza walipoteza, kama kocha alishangilia ushindi kwa sababu ya Utanzania wake.
“Watu walishangaa kwa nini nilishangilia, mimi nilikuwa namuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wake Philip Mpango lakini pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambao kwa pamoja wametoa sapoti kubwa kwenye michezo,” alisema Julio.
“Naamini Simba wataenda kufanya kama ilivyotokea kwa Zamalek ambapo walishinda 1-0 nyumbani lakini wakapoteza 1-0 Misri tukawatoa kwa penalti baada ya kipa Juma Kaseja kuokoa penalti mbili zilizoivusha timu hatua inayofuata,” alisema Julio.
Alisema anampongeza mwekezaji wa Simba Mohamed Dewji kwa kazi kubwa aliyoifanya hata kama kuna mapungufu ya kibinadamu kwani kwenye ubora wa Simba amechangia kiasi kikubwa kufika pale ilipo.
“Lakini pia nimpongeze Ghalib Mohamed na Rais wa Yanga, Hersi Said wamefanya kazi kubwa kuitoa Yanga ilikokuwa kwa kufanya usajili bora na kuitengeneza timu ya ushindani ambayo inawafurahisha Watanzania wote hadi Rais Samia,” alisema Julio.
Simba itacheza keshokutwa Ijumaa dhidi ya Wydad kwenye Uwanja wa Mohamed V, jijini Casablanca wakati Yanga itakuwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Jumapili hii kuvaana na Rivers.
