Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imekiri kuwa na kibarua kigumu kuelekea mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Ruvu Shooting, ikikiri ni mchezo mgumu kwao kulingana na mazingira ya timu zote mbili.
Kocha Msaidizi wa Azam, Aggrey Morris amesema wanauchukulia mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa umakini mkubwa kutokana na nafasi iliyopo Ruvu wakitambua namna gani wapinzani wao wanauhitaji ushindi.
“Mchezo tunaocheza na Ruvu ni mchezo tunaouchukulia kwa umakini mkubwa, ukiangalia msimamo ulivyo, siku zote ukicheza na timu ya hali kama hii ndiyo inaogopesha kabisa, hilo tunalijua, tunaiheshimu ni timu ya ushindani, upinzani utakuwa mkubwa lakini tumejipanga kufanya vizuri,” alisema Aggrey.
Azam yenye pointi 50 katika nafasi ya nne, inautafuta ushindi kuipiku Singida BS iliyo nafasi ya tatu kwa pointi 51 wakati Ruvu iliyo nafasi ya 15 kwa pointi 20 inapambana kujinasua isishuke daraja.
Ofisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire ameeleza kuwa wanatambua ugumu wa mechi hiyo kutokana na mahitaji ya timu zote mbili lakini mipango yao ni kutumia mechi nne zilizobaki kujinasua na janga la kushuka daraja hivyo anafahamu ugumu utakaokuwepo.
“Azam wanatafuta nafasi ya tatu ili pengine iwe rahisi kushiriki mashindano ya Caf (Shirikisho la Soka Afrika), na sisi tunapambana kuhakikisha tunashinda mechi zilizosalia ili tuendelee kuwepo kwenye ligi msimu ujao na hatuhitaji kupoteza mechi hizi, kuna marekebisho mengi tumefanya kuhakikisha tunasalia,” alisema Bwire.
Katika mechi tano za mwisho za ligi, Azam imeshinda mbili, sare moja na kufungwa mbili wakati Ruvu imeshinda michezo miwili na kufungwa mitatu. Mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo msimu huu iliisha kwa sare ya mabao 2-2.
Mechi nyingine ya ligi itakayopigwa kesho itazikutanisha Dodoma Jiji dhidi ya KMC Uwanja wa Jamhuri Dodoma. Mechi ya kwanza, KMC ilishinda kwa bao 1-0.
Soka Azam, Ruvu Shooting vitani
Azam, Ruvu Shooting vitani
Read also
