Na mwandishi wetu
Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson na wabunge wa Mbeya wameipa Sh 3,000,000 timu ya Mbeya City kama motisha kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Kagera Sugar.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Jumanne mjini Dodoma wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na Spika kwa ajili ya timu hiyo iliyokuwa safarini ikielekea Bukoba kwa mechi yao hiyo itakayopigwa Aprili 23, mwaka huu.
Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka aliyewakilisha wabunge wengine kutoa pesa hizo alisema katika mchanganuo wa kiasi hicho, Dk Tulia ametoa Sh 2,000,000 huku wabunge wengine wa Mbeya wakichanga kiasi cha Sh 1,000,000.
“Tumekutana na timu kuwapa motisha kuhakikisha wanafanya vizuri kuepuka kushuka daraja kulingana na nafasi waliyopo, tumeona tuwachangie pesa kidogo kuchangia ushindi na pia tukazungumza nao kwamba kuanzia sasa tutanunua ushindi katika mechi zote zilizobaki,” alisema Kasaka.
Alisema kuwa hamasa hiyo itafanyika pia kwa viongozi wengine wa Mbeya kuanzia mechi ijayo, hiyo ni kuhakikisha timu hiyo ambayo ni kama nembo ya wananchi wa Mbeya haishuki daraja mwisho wa msimu huu.
Ahadi na motisha hizo zimeendelea kumiminika baada ya hivi karibuni aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kueleza kuwa atakuwa akinunua ushindi wa timu hiyo kwa Sh 1,000,000 katika mechi nne zilizosalia.
City inashika nafasi ya 13 kwa pointi 27 baada ya mechi 26 ambapo ukiachana na Kagera Sugar, imebakiza pia kuumana na Geita Gold, Yanga na KMC kabla ya kufungwa rasmi pazia la ligi.
Soka Spika, wabunge waichangia Mbeya City
Spika, wabunge waichangia Mbeya City
Read also
