Na mwandishi wetu
Timu ya Simba inaingia kambini leo Jumanne jioni kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mchezo wa robo fainali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya mabingwa watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco.
Mchezo huo umepangwa kupigwa Aprili 22, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuanzia saa 10 jioni.
Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa kwa sasa akili zao wamezielekeza kwenye mchezo huo lengo lao likiwa ni kuitumia vizuri faida ya kuanza nyumbani kwa kuvuna ushindi mnono utakaowaweka sehemu salama kwenye mchezo wa marudiano.
“Baada ya mchezo wetu dhidi ya Yanga, tulitoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji na leo wanaingia kambini tayari kujiandaa na mchezo huo ambao kocha wetu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ametuhakikishia ushindi kwa maandalizi ambayo watayafanya hadi kufika siku ya mchezo,” alisema Ally.
Meneja huyo ameeleza kuwa katika kuhakikisha ushindi unapatikana kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga, uongozi wao unapambana kuhakikisha maandalizi yao yanafanyika katika ubora wa hali ya juu ikiwemo kuwatimizia wachezaji na benchi la ufundi kila wanachokihitaji.
Alisema wanatambua kuwa hautokuwa mchezo mwepesi kutokana na ubora wa wapinzani wao Wydad lakini wamejipanga kuhakikisha wanautumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kupata ushindi.
Ally pia alisema wapinzani wao watawasili nchini Alhamisi wakiwa na msafara wa watu wasiopungua 50 pamoja na viongozi wa timu na benchi la ufundi .
Soka Simba yaingia kambini ikiisubiri Waydad
Simba yaingia kambini ikiisubiri Waydad
Read also
