Barcelona, Hispania
Rais wa Barcelona, Joan Laporta amesema kwamba uchunguzi unaofanywa kuhusu tuhuma za klabu hiyo kudauwa kumhonga makamu rais wa zamani wa kamati ya waamuzi ni kampeni za kuichafua klabu hiyo.
Katika mkutano aliofanya na waandishi wa habari leo Jumatatu, Laporta alisema kuna kampeni chafu dhidi ya Barca huku akimtupia lawama bosi wa La Liga, Javier Tebas na kushindwa kuielewa klabu ya Real Madrid kwa kuingilia kesi dhidi ya klabu hiyo.
Barca inadaiwa kumlipa makamu mwenyekiti wa kamati ya waamuzi, Jose Maria Negreira, Euro milioni 7 kati ya mwaka 2001 na 2018, malipo ambayo yalifanywa kupitia kampuni inayomilikiwa na Negreira.
Waendesha mashitaka wanadai kuwa malipo hayo yamefanywa na Barca ili klabu hiyo ipewe upendeleo lakini Laporta amedai kuwa malipo hayo yalitolewa kwa ajili ya kutaka ripoti ya ufundi ya waamuzi kuhusu uchezeshaji wa mechi.
“Barcelona haijawahi kuwa na nia ya kutoa ushawishi au kuingilia mashindano ili kupendelewa kwa namna yoyote kwenye michezo,” alisema Laporta.
“Mahakama hazijapata ushahidi wowote au vinginevyo kwa sababu ushahidi huo haupo, na haiwezekani, haya ni matokeo ya kampeni za kuichafua Barcelona,” alisisitiza Laporta.
“Ni mashambulizi machafu dhidi ya Barcelona na yamekuwa yakifanywa ili kutuyumbisha na kuharibu heshima ya klabu,” aliongeza.
Laporta pia alisema wameshachukua hatua za kisheria dhidi ya hilo na tayari wamewasilisha mashtaka 20 kwenye vyombo vya sheria dhidi ya waandishi wa habari na watu wengine kwa makosa ya udhalilishaji.
Mbali na klabu ya Barca na Laporta, watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni marais wa zamani wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) nalo limeahidi kufanya uchunguzi wake kuhusu kashfa hiyo.
