Na Hassan Kingu
Kesho Jumapili shughuli za wapenda soka zitasimama kwa dakika 90 kupisha mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga ambazo zinakutana zikiwa tayari zimedhihirisha ubora katika ligi ya ndani na Afrika.
Timu hizo za jijini Dar es Salaam zinakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi inayotarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili kwa sasa na matokeo yao ya mechi za nyuma za ligi na Kombe la FA.
Utamu zaidi pia ni upinzani uliopo baina ya timu hizo ambazo zinakutana Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC kwa pointi 68 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 60 baada ya wote kucheza mechi 25.
Kwa kifupi matokeo ya mechi hiyo yatatoa taswira juu ya ubingwa msimu huu kwani Yanga ikishinda itakuwa imebakiza takribani pointi sita itangaze ubingwa lakini ikiwa tofauti Simba itakuwa na mwanya wa kuendelea kumkimbiza ‘mwizi’ kimyakimya.
Simba ambayo iliutwaa ubingwa wa ligi mara nne mfululizo kabla ya kupokonywa na Yanga msimu uliopita, itahitaji kupambana kutotoa nafasi ya kuwa kama daraja la Yanga kutetea taji hilo msimu huu.
Mbali na wababe hawa wanaotawala msimamo kukutana wenyewe kwa wenyewe lakini pia hata namba za juu za mabao wametawala wao, hivyo ufundi na upinzani mkubwa unatarajiwa kesho.
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele anaongoza orodha ya mabao Ligi Kuu NBC kwa kufunga mara 16 lakini kwenye orodha ya vinara wa pasi za mwisho, jina la kiungo wa Simba, Clatous Chama lipo nafasi ya kwanza kwa pasi zake 14.
Ubora wao katika msimamo na kwenye orodha za tuzo binafsi inaonesha ni kwa kiasi gani timu zote zimekuwa na matokeo mazuri kwenye ligi msimu huu.

Mpaka sasa Yanga imefungwa mechi moja na kutoa sare mbili, Simba nayo imefungwa mechi moja na kutoa sare mara sita. Kiujumla ndio timu mbili pekee zilizofungwa mechi moja moja ambazo ni chache zaidi msimu huu.
Kuthibitisha umwamba wao, timu hizo kwenye mechi zake mbili za mwisho zimeshinda kibabe na kutuma salamu kwa mwenzake.
Yanga iliitungua Geita Gold kwa bao 1-0 na kutinga nusu fainali ya Kombe la FA kabla ya kuifumua Kagera Sugar mabao 5-0 kwenye ligi, Simba nayo iliibamiza Ihefu mabao 5-1 kukata tiketi yao ya nusu fainali Kombe la FA.
Kama haitoshi ikaichapa tena mabao 2-0 kwenye mechi iliyofuata ya ligi na kuvunja ubabe wa Ihefu kuzidhibiti timu vigogo kwenye uwanja wake wa nyumbani kama ilivyofanya kwa Yanga, Azam, Mtibwa Sugar na Singida Big Stars.

Katika mechi hizo, timu zote zimejaribu kuweka silaha zake sawasawa kwa kutumia wachezaji ambao pia walikuwa hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara na hesabu hizo kutoa matokeo mazuri kutokana na viwango walivyoonesha.
Mechi ya Caf kupigwa Dar
Ukiachana na ubabe wao wa michuano ya ndani ya nchi lakini pia timu hizi zinapeperusha vyema bendera kwenye michuano ya klabu Afrika, zimedhihirisha ubora na umahiri wao Afrika.
Zote zimetinga robo fainali na hii ni mara ya kwanza kwa timu za Tanzania kufanya hivyo, Simba itavaana na Wydad Casablanca ya Morocco kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga itakuwa na kibarua dhidi ya Rivers United ya Nigeria kwenye Kombe la Shirikisho.
Zimefika hapo kwa kuonesha ufundi na kuvuja jasho kwelikweli na mwisho zimewapa furaha mashabiki wake, sasa ubora wao huo waliouonesha dhidi ya wababe wengine wa michuano ya Caf unatarajiwa kuoneshwa kwenye mechi ya kesho.
Wengi wanatarajia kuona soka safi na la kuvutia lenye pasi zinazoonekana na kuchezwa kwa ufundi na ubabe unaotakiwa wenye viwango vya ‘derby’ kweli ya Kariakoo kama si ya Tanzania au Afrika Mashariki na Kati.
Umaarufu wa mechi hii hauishii Afrika Mashariki pekee kwani kwa soka waliloonesha msimu huu, hata Morocco, Nigeria na kwingineko watataka kufahamu nini kitajiri ndani ya dakika hizo 90.
Wapinzani wa timu hizo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho wote watakuwa wanaifuatilia mechi hii si kwa kutaka tu kujua matokeo bali kuendelea kusoma ubora wa timu hizo na kuweka mikakati yao.
Kulingana na ubora unaotarajiwa, upana wa vikosi na namba kubwa walizonazo kwenye michuano yote wanayoshiriki msimu huu ni wazi itakuwa mechi yenye hadhi ya juu itakayopigwa Dar es Salaam itakayofuatiliwa na Waafrika wengi.
Mtihani mwingine kwa Robertinho
Kesho ni mechi ya 10 baina ya wababe hao kukutana mfululizo katika misimu ya hivi karibuni na katika mechi tisa zilizopita, Simba imeshinda mara moja, Yanga mara tatu na zilizobaki ni matokeo ya sare.
Ni kama vile Simba inautafuta ushindi kwa muda mrefu dhidi ya Yanga na inaamini kwa kikosi ilichonacho na moto walionao na huu ndio wakati sahihi wa kufanya hivyo chini ya kocha Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Kwa bahati mbaya hii ndio derby ya kwanza kwa kocha huyo tangu atue kuinoa Simba Januari, mwaka huu akitokea Vipers ya Uganda.
Na baada ya awali kuuvuka mtihani wake wa kuipeleka Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kama ilivyokuwa ikifanywa na watangulizi wake, sasa ana kibarua kingine cha kuondoa ukame wa ushindi Msimbazi dhidi ya Yanga.

Ingekuwa miaka michache nyuma, pengine ingekuwa rahisi kutabiri hatma ya kibarua cha Robertinho baada ya kufungwa kwenye mchezo huo lakini angalau mambo sasa yamebadilika na mechi zimepunguza presha kwa makocha japo bado zina joto kali na linahitaji umwamba kulivumilia.
Robertinho anayesaidiwa na Juma Mgunda atapambana na Nasreddine Nabi ambaye amezizoea mechi hizi kutokana na kudumu kwake Yanga akiwa na kikosi hicho kwa muda mrefu, akishiriki kwa asilimia kubwa kukijenga mpaka sasa.
Lakini uzuri au ukakasi wa mechi za Simba na Yanga, matokeo yake hayajawahi kutabirika tangu kugundulika kwa timu hizo takribani miaka 87 iliyopita, bila kujali timu ipi mbovu na ipi nzuri kwa wakati husika.

Hivyo, japo Robertinho ni mgeni kwenye derby hii lakini bado anaweza akafanya jambo kama mwenyewe alivyojinasibu kuwa mechi kama hizo ndio mechi zake na alishapambana nazo hata wakati anazinoa klabu za Uganda na Rwanda kwa nyakati tofauti.
Vita ya Baleke, Mayele
Pamoja na yote lakini nyasi zitapata shida kwa mabeki kujaribu kuwadhibiti Mayele na mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke ambaye amekuwa na kiwango cha juu mno katika mechi za hivi karibuni.
Mayele anatambulika ubora wake, msimu uliopita alifunga mabao 16 kwenye ligi na msimu huu tayari ameshaifikia idadi hiyo. Ana njaa ya mabao, anatembea na mpira, anapiga chenga na anafunga kwa juhudi kubwa mno.
Ujio wa Kennedy Musonda Jangwani umeongeza kitu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, kasi na njaa yake ya kufunga imekuwa lulu mpya kwa Yanga, uwepo wa Stephane Aziz Ki ni gumzo lingine.
Baada ya kukaa nje kwa muda, Aziz Ki alirejea kwenye mechi yao dhidi ya Kagera na kuonesha kiwango kikubwa akifunga ‘hat-trick’na kufikisha mabao manane.
Bernard Morrison ambaye naye alikuwa nje kwa muda akisumbuliwa na majeraha amerejea kwenye mechi hiyo na kufunga bao.

Uwepo wa Jesus Moloko na Tuisila Kisinda pia ni jambo jingine kwa safu ya ulinzi ya Simba. Wawili hawa sio wafungaji wa mara kwa mara lakini wamekuwa na mchango mkubwa wa upatikanaji mabao kutokana na pasi na krosi zao murua kutokea pembeni mwa uwanja.
Wakati Mayele na wenzake wakiendelea na kazi zao, upande wa pili Simba inatamba kwa uwepo wa Baleke ambaye taarifa zake zinasikika kila kona kwa ufundi wake wa kufunga, kukaa kwenye nafasi, kulaghai mabeki na kadhalika.
Ni hivi, Baleke tangu atue Januari, mwaka huu amefunga mabao manne kwenye mechi mbili za Kombe la FA, amefunga mabao matatu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na kwenye Ligi Kuu NBC mpaka sasa amefunga mabao saba.
Pamoja ya kwamba, Saido Ntibazokiza amefunga mabao 10, akimfuatia Mayele kwenye orodha ya wafungaji lakini kasi ya ufungaji ya Baleke inazua gumzo kuelekea mechi hiyo.
Moses Phiri ambaye tangu amerejea kutoka majeruhi bado hajaanza kutumika ipasavyo pia anapigiwa chapuo kuichachafya ngome ya Yanga kama atapata nafasi, akiwa na mabao yake 10 pia mpaka sasa.
Winga Pape Sakho na Kibu Denis ni washambualiaji wengine wenye kasi na faida kwa Simba, inapotokea wameingia kutokea benchi au wameanza, huwa si wafungaji wa mara kwa mara kama hao wengine niliowataja lakini nao wanaweza kusababisha lolote wakati wowote.

Mwisho wa yote, mechi hii inatarajiwa kuwa na matokeo ya mabao tofauti na mechi za timu hizi zilizopita kwani msimu huu kwenye ligi zimefungwa ‘hat-trick’ mara saba.
Ibrahim Mkoko wa Namungo amefunga moja, Mayele na Aziz Ki kila mmoja amefanya hivyo mara moja kama alivyofanya Chama, Ntibazonkiza na Baleke wakati John Bocco akiwa amefanya hivyo mara mbili na kwenye orodha ya wafungaji ana mabao tisa.
Kuna ambao wameanza kupata hisia kwamba huenda rekodi ya hat-trickya miaka zaidi ya 40 iliyopita katika mechi za Simba na Yanga anayoishikilia Abdallah Kibaden wa Simba ikapata mtu mwingine katika mechi hii, ni jambo gumu lakini si la kulifuta kabisa.
Kwa kifupi inatarajiwa kuwa mechi ya kibabe iliyojaa ufundi mwingi wa kushindana kufunga na ujio wa Baleke umeongeza moto wa mechi hiyo na pengine tutashuhudia mechi ya zaidi ya sare ya bao 1-1, matokeo ambayo tuliyashuhudia kwenye mechi ya kwanza ya mapacha hao msimu huu.