Na mwandishi wetu
Ligi ya mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL) inatarajiwa kuanza kuunguruma Mei 6, mwaka huu ambapo itashirikisha timu za wanaume na za wanawake ambazo safari hii zitakuwa 12.
Akizungumza leo Jumamosi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kamisheni ya Mipango, Maendeleo na Masoko wa Chama cha Kikapu Dar, Terence Mhumbira alisema kuwa msimu huu kuna timu mbili za wanawake zimeongezeka na kwamba tayari maandalizi yameshaanza.
Ameeleza kuwa jina la ligi hiyo litabadilika kutoka RBA hadi BDL akisema wameangalia sababu za kibiashara huku wakitarajia ushindani mkubwa kutokana na aina na timu zilizopo na usajili wao.
“Tuko kwenye maandalizi ya ligi ya mkoa wa Dar es Salaam tukitarajia itakuwa ya kiwango cha juu kutokana na timu zilizopo, washiriki wanatakiwa waanze maandalizi ili kuleta ushindani na mwisho wa siku kupata wawakilishi bora wa kushiriki ligi ya taifa,” alisema Mhumbira.
Timu za wanawake zitakazoshiriki ni DB Lioness, JKT Stars, Jeshi Stars, Kurasini Dibas, Mchenga Queens, Pazi Queens, Ukonga Queens, Vijana Queens, UDSM Queens, Polisi Queens, Oilers Princess na Magereza.
Kwa upande wa timu za wanaume ni ABC, Chui, Dar City, DB Oratory, JKT, Jogoo, Mchenga, Mgulani, Oilers, Pazi, Polisi, Savio, UDSM Outsiders, Ukonga Kings, Ukonga Warriors na Vijana City Bulls.